1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uturuki yaitaka Saudi Arabia kuutoa mwili wa Jamal Khashoggi

26 Oktoba 2018

Rais wa Uturuki amesema muendesha mashitaka wa Saudi Arabia anatarajiwa kuwasili nchini humo siku ya Jumapili kuzungumza na maafisa wa serikali yake ikiwa ni sehemu ya uchunguzi kuhusu mauaji ya Jamal Khashoggi.

https://p.dw.com/p/37G7p
Türkei | Fall Khashoggi
Picha: picture-alliance/dpa/abaca/Depo Photos

Tangazo la rais Recep Tayyip Erdogan linakuja siku moja baada ya muendesha mashitaka huyo  wa Saudi Arabia kusema kutokana na ushahidi uliotolewa na Uturuki, mauaji ya Jamal Kashoggi yalipangwa. hii ikiwa ni mara ya kwanza kwa taifa hilo kutoa tamko kama hilo juu ya mauaji ya hayo.

Kuuwawa kwa Kashoggi tarehe 2 Oktoba mwandishi wa gazeti la Marekani la Washington post na mkosoaji mkubwa wa sera za mrithi wa Saudi Arabia Mohammed bin Salman maarufu kama MBS kumesababisha lawama kali dhidi ya utawala wa Saudi Arabia.

Jamal Khashoggi
Mwandishi habari alieuwawa Jamal Khashoggi Picha: picture-alliance/AP Photo/V. Mayo

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan ametoa wito kwa ufalme wa Saudia kuweka wazi ni nani hasa alieamuru mauaji ya muandishi habari Jamal Khashoggi. "Lazima muoneshe mwili wake," alisema Erdogan wakati alipokuwa anawahutubia wanachama wa chama chake mjini Ankara hii leo.

Mwandishi habari  huyo aliekuwa  na miaka 59  amekuwa akiishi uhamishoni nchini Marekani tangu mwaka 2017. Aliuwawa baada ya kuingia Ubalozi mdogo wa Saudi Arabia mjini Istanbul tarehe mbili mwezi huu  ili kupata stakabadhi aweze  kumuoa mchumba wake raia wa Uturuki.

Ujerumani yasema itasimamisha mauzo ya silaha kwa Saudi Arabia  mpaka uchunguzi ukamilike juu ya mauaji ya Khashoggi

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel ameapa kusimamisha mauzo ya silaha kwa Saudi Arabia hadi pale maelezo ya kina yatakapotolewa juu ya mauaji ya mwandishi habari Jamal Khashoggi.

Nae rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amesema kusimamisha mauzo hayo kwa sababu ya mauaji ya mwanahabari huyo ni hatua isiyofaa. Kwa sasa falme hiyo imewatia nguvuni maafisa wake 18 wanaoshukiwa kuhusika na mauaji hayo.

Deutschland Bundestag
Kansela wa Ujerumani Angela MerkelPicha: Reuters/H. Hanschke

Huku hayo yakiarifiwa mtaalamu wa Umoja wa Mataifa Agnes Callamard alisema hapo jana kwamba Kashoggi ni muathirika wa mauaji yalio kinyume cha sheria yaliotekelezwa na Saudi Arabia huku akitaka uchunguzi wa kina kufanyika juu ya suala hilo.

Kulingana na shirika la kutetea haki za binaadamu la Human Rights Watch, mtotowa kiume wa Mwandishi  Jamal Kashoggi Salah Kashaoggi hatimae ameruhusiwa kuondoka nchini Saudi Arabia na kuelekea Marekani baada ya hatua ya kumpiga marufuku  kusafiri aliowekewa na falme hiyo.

Kuondoka kwake kulikuja baada ya kuonekana kwenye picha akipeana mkono na mrithi  wa Ufalme Mohammed Bin Salman huku akimtazama kwa ujasiri

Mwandishi: Amina Abubakar/AFP/AP

Mhariri: Mohammed  Abdul-Rahman