Uturuki yakasirishwa na kauli ya Merkel
17 Agosti 2017Kansela wa Ujerumani Angela Merkel kusema kuwa hakutakuwa na upanuzi wa chama kinachohusika na forodha wala kuimarisha mahusiano kati ya Umoja wa Ulaya na Uturuki
Mvutano hasa kati ya Uturuki na Ujerumani umekuwa mkubwa kwa sababu maafisa wa Uturuki waliwazuia raia kadhaa wa Ujerumani akiwemo Mwandishi wa habari na mwanaharakati wa haki za binaadamu.
Ujerumani pia inaondoa wanajeshi wake kutoka kituo cha jeshi la anga cha Incirlik baada ya Uturuki kuwazuia wanasiasa wa Ujerumani kuzuru kituo hicho. Uturuki bado inawania kujiunga na Umoja wa Ulaya lakini Merkel amesema jana kuwa hakuna kurasa mpya zinazofunguliwa katika mazungumzo ya uwanachama wan chi hiyo na kuwa msaada kwa Uturuki umepunguzwa kwa kiasi kikubwa.
Lakini waziri wa Uturuki kuhusu Umoja wa Ulaya Omer Celek amesema matamshi ya Merkel hayafai na yenye kuharibu. "tunapaswa kusisitiza kuwa hakuna mwanachama wa EU anayepaswa kutoa maagizo kwa taasisi au michakato ya EU. Namna Umoja wa Ulaya unavyochukua maamuzi yake na namna taasisi zinavyofanya kazi ni kitu cha kanuni. bahati mbaya, hali hii ni hatari sana, zinawakilisha kauli zinazoweza kuumiza uadilifu wa EU".
Akizungumza na wanahabari mjini Ankara, Celik amesema Uturuki na Umoja wa Ulaya zitafaidi kwa kukiimarisha chama cha forodha. Tazama ripoti zinazochapishwa na EU kuhusu uchambuzi wa athari. Uturuki na EU zote zinaweza kunufaika kwa kukiimarisha chama cha forodha. EU inajifanya kana kwamba kuimarisha Chama cha Forodha ni kitu cha neema. ni vibaya sana. Hakuna haraka.
Ujerumani, taifa linaloongoza kiuchumi barani Ulaya, limekaza msimamo wake dhidi ya Uturuki katika wiki za karibuni, na kuwaomba raia wake kuchukua tahadhari kama wanasafiri kwenda nchini humo na ikatishia kuchukua hatua zinazoweza kuathiri uwekezaji wa Ujerumani.
Rais Recep Tayyip Erdogan amesema msako wa baada ya jaribio la mapinduzi, ambapo watu 50,000 wanazuiliwa na wengine 150,000 kufutwa kazi au kusimamishwa kutoka sekta za mahakama, habari, elimu na sekta nyingine, ulihitajika ili kushughulikia vitisho vikubwa vya usalama nchini humo. Wakosoaji wa ndani na nje ya Uturuki wanamtuhumu kwa kutumia hali ya hatari kama mbinu ya kuuangamiza upinzani na kujiimarisha madarakani.
Celik ameitaka Ujerumani kushirikiana kuhusu ombi la Uturuki la kumrejesha nyumbani Adil Oksuz, mhadhiri wa masuala ya kidini anayeshukiwa kuwa na mchango mkubwa katika jaribio la mapinduzi lililoshindwa. Celik amerudia malalamiko ya Uturuki kuwa iliwasilisha maelfu ya faili kwa Ujerumani na kuomba washukiwa wa jaribio la mapinduzi wakabidhiwe Uturuki lakini haijapata majibu yoyote kutoka Berlin. Ujerumani inakanusha tuhuma kuwa haishirikiani na maombi ya Uturuki.
Mwandishi: Bruce Amani/Reuters
Mhariri: Josephat Charo