Uturuki yaondolewa katika mpango wa ndege chapa F-35
18 Julai 2019Msemaji wa Ikulu ya Stephane Grisham amesema katika taarifa kuwa uamuzi wa Uturuki kununua mfumo wa Urusi wa S-400 wa kukinga makombora unafanya ushiriki wake katika mafunzo ya ndege chapa F-35 kushindikana.
Ndege hizo zilizotengenezwa nchini Marekani chapa F-35 , haziwezi kufanyakazi pamoja na jukwaa la ukusanya taarifa za kiintelijensia la Urusi ambalo litatumika kujifunza juu ya uwezo wake wenye mbinu za kisasa zaidi, amesema Stephanie Grisham.
Wizara ya mambo ya kigeni ya Uturuki imeieleza hatua hiyo kuwa si ya haki, ikisema katika taarifa kuwa , hatua hii ya upande mmoja haiendi pamoja na moyo wa ushirikiano wa jumuiya ya NATO na wala haiko katika misingi ya sababu halali.
Grisham amesema kuwa Marekani imetoa maombi kadhaa ya mfumo wake wa ulinzi dhidi ya makombora wa Patriot kwa Uturuki, lakini Ankara iliendelea na ununuzi wa mfumo wa S-400, unaokwenda kinyume na ahadi za ANTO kuepusha kutumia mifumo wa Urusi.
"Hatua hii itakuwa na athari kubwa kwa Uturuki katika operesheni zake na jumuiya ya NATO," amesema. Grisham ameongeza kuwa Marekani "bado inadhamini sana" uhusiano wake wa kimkakati na Uturuki na itaendelea kushirikiana nayo kwa kiasi kikubwa, kwa kutafakari juu ya utata uliopo kutokana na kuwapo na mfumo wa S-400 nchini Uturuki.
Mfumo wa S-400
Tangazo hilo limekuja siku tano baada ya Uturuki kuanza kupokea mfumo wa makombora wa Urusi , ikikaidi miaka miwili ya onyo kutoka Marekani na mataifa mengine washirika wa NATO kwamba hatua hiyo inaweza kuathiri uhusiano wao.
Hatua ya marekani itayatenga makampuni kadhaa ya Uturuki yanayotengeneza baadhi ya sehemu na vipuri vya ndege za kijeshi chapa F-35, na kuzuwia mipango ya Uturuki kununua ndege hizo 100 za kivita.
Siku ya Jumanne , rais Donald Trump alikataa kuishutumu Uturuki kutokana na kununua mfumo huo wa S-400, akisema kuwa rais Recep Tayyip Erdogan amelazimika kuchukua hatua hiyo na mtangulizi wake katika Ikulu ya Marekani Barack Obama.
Hali hii itakuwa ni upotevu mkubwa wa mapato kwa kampuni ya marekani ya Lockheed Martin inayounda ndege hizo.
Uhusiano kati ya Uturuki na Marekani umeathirika kwa miaka kadhaa sasa, kwa sehemu fulani kutokana na mzozo nchini Syria, pamoja na ushirika wa marekani na wapiganaji wa Kikurdi nchini Syria ambao Ankara inawaona kuwa na magaidi. Wizara ya mambo ya kigeni ya Uturuki imesema Marekani inapaswa kuonesha kwamba inathamini uhusiano uliopo wa kimkakati , kwa kupambana dhidi ya makundi ya kigaid.