1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uturuki yapeleleza raia wake Ujerumani

Isaac Gamba
28 Machi 2017

Ujerumani imewatahadharisha waturuki waishio nchini humo, kuwa Uturuki inafanya upelelezi dhidi yao na kuwapiga picha kwa njia ya siri.

https://p.dw.com/p/2a6RO
Deutschland Fußball EM 2008 Flagge Türkei und Deutschland
Picha: AP

Vyombo vya habari vya Ujerumani vimeripoti kuwa idara za ujasusi za Uturuki zinawatuhumu mamia ya raia wa Uturuki waishio Ujerumani kuwa wafuasi wa  muhubiri wa kiisilamu Fethullah Gulen, na wamekusanya taarifa kuwahusu na kuzikabidhi kwa vyombo vya usalama vya Ujerumani.

Kwa mujibu wa gazeti la Suddeutsche Zeitung  taarifa hizo za upelelezi zina anuani, nambari za simu pamoja na picha zilizopigwa kwa njia ya siri kwa kutumia kamera za uchunguzi.   Zaidi ya watu 300, vilabu tofauti tofauti vipatavyo 200, shule pamoja na taasisi nyingine zinahusishwa kuwa na mahusiano na  Gulen anayeishi nchini Marekani.

Mkuu wa idara ya ujasusi nchini Ujerumani inayofuatilia masuala ya nje alikabidhiwa orodha hiyo na mwenzake wa Uturuki wakati wa mkutano wa kimataifa wa masuala ya usalama uliofanyika mjini Munich, lakini baadaye serikali ya Ujerumani iliwatahadharisha watu hao kuwa wanafuatiliwa na Uturuki.

Ofisi inayohusika na masuala ya uhalifu katika jimbo la North Rhine Westphalia nchini Ujerumani ilikwenda mbali zaidi na kuwaonya raia hao kuwa serikali ya Uturuki itachukua hatua dhidi yao pindi watakaporejea nchini humo.

Uturuki yamtuhumu Gulen kuhusika na jaribio la mapinduzi

USA Fethullah Gülen bei einer Pressekonferenz
Muhubiri wa kiisilamu Fethullah GulenPicha: picture-alliance/dpa/M. Smith

Serikali ya Uturuki inamtuhumu Gulen kwa kuratibu jaribio la mapinduzi lililoshindwa  mwezi Julai mwaka jana. Tangu wakati huo Uturuki imekuwa ikiendesha operesheni  dhidi ya wapinzani wa serikali  huku pia ikiwatuhumu wafuasi wa Gulen kuhusiana na jaribio hilo la mapinduzi  ambao wamekanusha kuhusika kwa njia yoyote ile na mipango ya mapinduzi au ugaidi.

Taarifa hizi zinakuja mnamo wakati raia wa Uturuki waishio Ujerumani wakianza kupiga kura kwa ajili ya kura ya maoni ya mwezi Aprili yenye lengo la kufanyia mabadiliko katiba ya nchi hiyo ili kumuongezea Rais wa nchi hiyo  Recep Tayyip Erdogan mamlaka zaidi iwapo mabadiliko hayo yataidhinishwa.

Wakosoaji wanasema iwapo mabadiliko hayo yatapitishwa basi utakuwa ndio mwisho wa demokrasia nchini humo. Mchakato wa kuelekea katika kura hiyo ya maoni umezorotesha uhusiano wa kidiplomasia kati ya Uturuki na Umoja wa Ulaya baada ya mataifa hayo kufuta mikutano kadhaa ambayo maafisa wa Uturuki walitaraji kufanya kampeni kwa ajili ya kuwahamasisha raia wa Uturuki wanaoishi katika nchi za ulaya kushiriki kura hiyo ya maoni.

Kiasi ya raia  milioni 1.4 wa Uturuki wanaoishi Ujerumani wana vigezo vya kupiga kura katika zoezi hilo la kura ya maoni. Kansela wa Ujerumani Angela Merkel alimkosoa hadharani Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan baada ya kiongozi huyo kuzishutumu Ujerumani na Uholanzi kuwa zinajihusisha na  sera za kinazi kufuatia hatua ya nchi hizo kuwazuia mawaziri wa Uturuki wasiendeshe mikutano hiyo ya kampeni katika kuelekea kura hiyo ya maoni.

Mwandishi : Isaac Gamba/DW (Süddeutsche Zeitung, AFP, Reuters)

Mhariri      : Gakuba, Daniel

http://www.dw.com/en/turks-in-germany-warned-over-surveillance-from-ankara-report/a-38151664