Uturuki yazitaka Iran, Urusi kukomesha mashambulizi Syria
23 Februari 2018Makundi makubwa ya upinzani nchini Syria yanaitaka jumuiya ya kimataifa iizuwie Urusi isiwe sehemu ya wapigaji kura kwa azimio jipya la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, yakisema kuwa Urusi yenyewe ni sehemu ya mauaji yanayoendelea nchini Syria.
Salwa Aksoy, makamu rais wa Muungano wa Kitaifa wa Syria (SNC) amewaambia waandishi wa habari nchini Uturuki kwamba kwa mujibu wa mkataba wa Umoja wa Mataifa, mataifa ambayo ni sehemu ya mzozo hayana haki ya kupigia kura mswaada wa rasimu ya azimio linalohusiana na mzozo huo.
Urusi imekuwa muungaji mkono mkubwa wa Rais Bashar Assad na imejiunga naye kwenye vita tangu mwaka 2015, hatua ambayo inatajwa kuurejeshea nguvu mpya utawala wa Syria.
Sweden na Kuwait zinataka azimio hilo liamuru siku 30 za usitishwaji mapigano ili kuyaruhusu mashirika ya misaada kuwafikia watu na pia kuwahamisha wagonjwa na majeruhi kutoka maeneo yaliyozingirwa.
Mjumbe wa Umoja wa Mataifa ataka mapigano yasimamishwe
Kwa mujibu wa msemaji wa mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kwa Syria, Steffan de Mistura, Alessandra Vellucci, kupitishwa kwa azimio hilo kuna umuhimu ili kuiepusha Ghouta Mashariki kugeuka kama ilivyokuwa Aleppo.
"Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa anatoa tena wito kwa wale wenye dhamana ya kuyalinda makubaliano ya Astana kuitisha mkutano wa haraka ili kurejesha hali ya kawaida. Ameonya kwamba hali haiwezi kuachiwa ikawa kama ya Aleppo," alisema Vellucci.
Lakini Balozi wa Urusi kwenye Umoja wa Mataifa, Vassily Nebenzia, ametuma mapendekezo ya dakika za mwisho, huku akisema kuwa azimio hilo haliakisi uhalisia.
Katika hatua nyengine, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki, Mevlut Cavusoglu, amezitaka Urusi na Iran kukomesha mara moja mashambulizi dhidi ya Ghouta Mashariki, na badala yake ziuzuwie utawala wa Syria kuwauwa watu wake.
Urusi, Uturuki na Iran, kwa pamoja, ziliwahi kufikia makubaliano ya kuanzisha mchakato wa amani kwa kutenga maeneo yasiyoruhusika kuwa na mapigano nchini Syria, ikiwemo Ghouta Mashariki na jimbo la Idlib linaloshikiliwa na waasi.
Cavusoglu amesema mashambulizi yanayoendelea sasa kwenye maeneo hayo ni kinyume na makubaliano ya pande hizo tatu.
Mwandishi: Mohamed Khelef/AFP/Reuters
Mhariri: Saumu Yussuf