Uwekezaji wa China waduwaza raia Zambia
Ushawishi wa China nchini Zambia umesambaa kwa kiwango kikubwa katika miaka ya karibuni. Uwekezaji mkubwa unaacha sintofahamu kwenye uchumi wa taifa hilo. Wazambia wengi wanabaki kuangalia tu uwekezaji wa China.
Reli ya Urafiki
Mradi wa Reli ya Tanzania-Zambia (TAZARA) ulipomalizika mwaka 1976, ulikuwa ni msaada mkubwa zaidi kutolewa na China na ishara ya misaada ya China kwa nchi za Afrika zilizopata uhuru. China ilituma karibu wafanyakazi 50,000 wa uhandisi na ufundi kufanya kazi TAZARA. Hata hivyo mradi huu mkubwa umeendelea kudhoofika tangu mwishoni mwa miaka ya 1990. Sasa treni husafirisha zaidi shaba kuliko watu.
Zama mpya, "ishara kubwa ya urafiki"
Zambia inajenga mradi mkubwa wa usafirishaji unaofadhiliwa na China wa kilomita 321, (kilomita 200) za barabara mbili kutoka Lusaka hadi Ndola. Ujenzi huo unafanywa na shirika la ujenzi la China Jiangxi kwa dola bilioni 1.2 ambazo ni za mkopo kutoka Benki ya Exim ya China. Katika sherehe ya kuzinfua mradi huo. Rais Edgar Lungu aliuta "ishara ya urafiki wa zama mpya kati ya China na Zambia."
Miradi ya "Tembo mweupe"
Mfano mwingine wa matumizi ya kiwango kikubwa ni ujenzi na upanuzi wa uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Kenneth Kaunda. Thamani jumla ya mradi huo unaoendelea unakadiriwa kuwa dola 360,000,000, lakini pia unafadhiliwa na Benki ya Exim ya China na unajengwa na shirika la China Jiangxi. Wazambia wengi wanauona ni wa kifahari na wameuita mradi wa "tembo mweupe" na usio na maana.
Huduma za kifedha kati ya China na Zambia
Benki ya China imefungua matawi yake kila mahali nchini Zambia. Imekuwa ikiendesha biashara ya fedha ya Yuan tangu mwaka 2011, kutoa huduma za kifedha kwa makampuni ya Kichina yanayotaka kuingia katika soko la Zambia. Hata hivyo, haijulikani iwapo benki hizo zinatoa mikopo kwa raia wa Zambia.
Wajiingiza kwenye biashara ya Shaba
Shaba ni bidhaa kuu inayouzwa nje ya Zambia na makampuni ya Kichina yamejiingiza sana kwenye biashara hiyo kwa mfano kwenye kampuni ya Chambishi Copper Smelter. Hata hivyo walipoteza wanunuzi wakubwa kama Glencore ya Uswisi, First Quantum ya Canada, Barrick, na Vendanta ya India. China hata hivyo iliongeza kwa kasi uwekezaji katika migodi na sasa ikiwa na uwekezaji wa $ milioni 832 huko Chambishi.
Wamiliki wa siri wa maduka ya rejareja ya Wachina
Zambia inaruhusu wageni kufanya biashara kwa jumla tu, si kwa rejareja. Licha ya sheria hii, DW iligundua kuwa maduka mengi katika mji mkuu wa Lusaka yalikuwa na wafanyabiashara wa Kichina, ambao huja mara chache kukusanya fedha. Wananchi wa Zambia huajiriwa kama wauzaji na maduka hayo huwa yamesajiliwa kwa majina yao.
Kuchukua ajira za wazawa
Kwenye soko hili la kuku lililopo mitaa ya mabanda ya Lusaka, wachuuzi waliiambia DW kwamba malori makubwa ambayo huleta kuku sokoni hapo yanamilikiwa na wawekezaji wa China. Hii huwakasirika wenyeji ambao wanasema Wachina wameharibu maisha yao na kuchukua ajira zao. Serikali ya Zambia imekanusha kuwa wawekezaji wa China walijihusisha na shughuli kama za kukuza kuku na mahindi ya kuchoma.