1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uzalishaji wa viwandani wapungua pakubwa Ujerumani

8 Juni 2020

Pato la kila mwezi linalotokana na uzalishaji wa bidhaa za viwandani nchini Ujerumani lilipungua hadi asilimia 17.9% mnamo mwezi Aprili.2020.

https://p.dw.com/p/3dSRy
Deutschland Bundeskanzlerin Angela Merkel Interview im ARD Hauptstadtstudio
Picha: picture-alliance/dpa/J. Macdougall

Kwa mujibu wa takwimu za serikali kwa kuzingatia hesabu za mwaka hadi mwaka, pato hilo lilipungua kwa asilimia 25.3%, takwimu hizo zinaashiria kupungua kwa mapato kwa kiwango kikubwa tangu mwaka 1991. Hali hiyo ni mbaya kuliko wachambuzi walivyotabiri hapo awali.

Ujerumani sawa na nchi nyingine ilichukua hatua kwa ajili ya kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona kabla kuanza kulegeza hatua hizo kuanzia mwezi April. Kuzorota kwa tija katika msingi wa mwezi hadi mwezi kuliongezeka mara mbili zaidi ya mwezi uliotangulia wa Machi.

Kwa mujibu wa idara ya Takwimu, na kwa kulinganisha mwezi Aprili mwaka huu na kipindi kama hicho mwaka uliopita, uzalishaji viwandani nchini Ujerumani ulipungua kwa asilimia 25.3. Idara hiyo imetilia maanani hasa sekta ya magari ambapo uzalishaji ulianguka kwa asilimia 74.6.

Serikali ya kansela Angela Merkel ilikubaliana kutenga kiasi cha Euro bilioni 130 ili kuufufua uchumi
Serikali ya kansela Angela Merkel ilikubaliana kutenga kiasi cha Euro bilioni 130 ili kuufufua uchumiPicha: picture-alliance/Zoonar/Wolfilser

Katika hatua ya kukabiliana na hali hiyo serikali ya kansela Angela Merkel ilikubaliana kutenga kiasi cha Euro bilioni 130 ili kuufufua uchumi. Pamoja na hatua hizo ni kutoa ruzuku kwa ajili ya ununuzi wa magari ya umeme na kupunguza kodi kwa muda.

Wiki iliyopita idara ya takwimu ilibainisha kuzorota kwa asilimia 6.9 kwa mchakato wa kuanzishwa kampuni mpya katika robo ya kwanza ya mwaka. Kampuni zipatazo 145,000 ziliathirika. Hali ilikuwa mbaya hasa kwa kampuni ndogo ndogo zilizozorota kwa asilimia 14.6.

Takwimu za mauzo ya nje zimeonyesha kupungua kwa asilimia 25.8 baada ya kuanguka kwa asilimia 15 mnamo mwezi machi.Wizara ya uchumi imesema kwiango cha chini kabisa kimefikiwa.Ujerumani imeibuka katika hali nzuri mnamo robo ya kwanza ya mwaka kulinganisha na nchi nyingine,licha ya kuingia katika mdororo wa uchumi. Tija ya uchumi ilipungua kwa asilimia 2.2.

Vyanzo:/RTRE/AFP/DPA/AP