1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Venezuela yaahirisha kiapo cha Chavez

9 Januari 2013

Venezuela imetangaza kuahirisha rasmi sherehe za kula kiapo cha Urais kutokana na hali ya kiafya ya muhusika; Rais Hugo Chavez kuendelea kuwa mbaya.

https://p.dw.com/p/17GJ2
****ARCHIVBILD****Venezuela's President Hugo Chavez, left, hugs a hospital worker, back to camera, during a visit to injured people after a refinery explosion at the Rafael Calle Sierra's public hospital in Punto Fijo, Venezuela, Monday, Aug. 27, 2012. A fire at the Amuay refinery spread to a third fuel tank on Monday nearly three days after a powerful explosion that killed 41 people and ignited the blaze, Vice President Elias Jaua said. (Foto:Ariana Cubillos/AP/dapd)
Hugo Chavez KrankenhausPicha: AP

Tangazo la kuahirishwa kwa kiapo hicho limetolewa jana jioni na serikali jambo ambalo linaonyesha kuwa huenda mwisho wa utawala wa miaka 14 rais Hugo Chavez umewadia. Kiongozi huyo msoshalisti alipaswa kula kiapo hapo kesho kama ilivyopangwa.

Akisoma barua mbele ya bunge Makamu wa Rias wa Venezuela Nicolas Maduro alisema "Kamanda wetu mheshimiwa rais anataka kutujulisha kuwa kulingana na ushauri wa kitabibu aliopewa, kipindi cha kujiuguza upasuaji aliofanyiwa inabidi kiongezeke zaidi ya tarehe 10 Januari. Kutokana na hali hiyo, hataweza kufika mbele ya bunge katika terehe hiyo".

Bunge lakubali kusogezwa mbele kiapo

Mapendekezo hayo yalipitishwa na bunge hilo linaloongozwa na wanasiasa wengi kutoka chama tawala cha Chavez na wachambuzi wanasema kuwa hatua hiyo imefikiwa ili kuonyesha uungaji mkono wao kwa kiongozi huyo.

Nicolas Maduro, Makamu wa Rais wa Venezuela
Nicolas Maduro, Makamu wa Rais wa VenezuelaPicha: AFP/GettyImages

Barua hiyo ilisema kuwa serikali itapanga tarehe nyingine ya kufanyika kwa kiapo hicho lakini haikutaja ni siku gani hasa na wala haikutoa kipindi maalumu ambacho Chavez atarejea kutoka Cuba anakopata matibabu.

Serikali ya Venezuela imeitisha maandaamano makubwa hapo kesho nje ya Ikulu ya nchi hiyo huku Marais wa mataifa washirika wa Chavez wakiahidi kulitembelea taifa hilo akiwemo Jose Mujica wa Uruguay na Evo Morales wa Bolivia. Naye Rais wa Argentina Cristina Fernandez ameahidi kumtembelea Chavez mjini Havana siku ya Ijumaa wiki hii.

Pingamizi la upinzani

Hata hivyo wabunge wa vyama vya upinzani wamepinga vikali uamuzi huo wakisema kuwa unakiuka misingi ya katiba ya taifa hilo. Wapinzani wamekuwa wakisisitiza kuwa Chavez ni lazima ale kiapo katika muda uliopangwa ama la aachie ngazi na kupisha uchaguzi katika kipindi cha siku 30 zijazo.

Venezuelan opposition Henrique Capriles mwanasiasa wa upinzani Venezuela
Henrique Capriles mwanasiasa wa upinzani VenezuelaPicha: Reuters

Kumekuwepo na mkanganyiko wa kisheria kutokana na katiba ya taifa hilo kutokuwa wazi juu ya nini kinapaswa kufanyika Chavez atakaposhindwa kula kiapo tarehe 10 Januari. Mahakama Kuu ambayo inashikiliwa na watu watiifu kwa Chavez imeandaa mkutano na vyombo vya habari hii leo ambapo inatarajiwa kueleza mipango ambayo itampa fursa Chavez kula kiapo mara atakapopata nafuu.

Chavez mwenye umri wa miaka 58 ambaye alikuwa askari kwenye taifa lake, hajasikika tangu afanyiwe upusaji kwenye fupa lake la nyonga tarehe 11 mwezi Desemba mwaka jana.

Mwandishi: Stumai George/Reuters/Ap

Mhariri: Daniel Gakuba