1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaVenezuela

Venezuela yasubiri matokeo ya uchaguzi wa rais

29 Julai 2024

Raia nchini Venezuela wanasubiri matokeo ya uchaguzi wa rais uliofanyika jana Jumapili ambao utaamua hatma ya chama cha kisoshalisti kinacholitawala taifa hilo la Amerika ya Kusini kwa zaidi ya robo karne.

https://p.dw.com/p/4iqI3
Rais Nicolas Maduro na mpinzani wake Edmundo Gonzalez
Rais Nicolas Maduro na mpinzani wake Edmundo Gonzalez.Picha: Gustavo Moreno/AP/Pedro R. Mattey/Anadolupicture alliance

Rais Nicolas Maduro anayewania muhula mwingine ana matumaini makubwa ya kupata ushindi licha ya kuimarika kwa uungwaji mkono wa upinzani ambao umelalamika juu ya hofu ya kuwepo dosari kwenye uchaguzi huo.

Kiongozi wa upinzani Maria Corina Machado amekuwa nyota wa kampeni ya muungano wa vyama vya upinzani licha ya yeye kuzuiwa kugombea wadhifa wowote wa uongozi nchini humo.

Marufuku hiyo ilimlazimisha Machado kumpatia nafasi Edmundo Gonzalez kuwa mgombea wa upinzani ili kuchuana na rais Maduro. Upinzani umesema unatilia mashaka uhuru wa uchaguzi huo hasa baada ya wafanyakazi wake kadhaa kukamatwa.

Hata hivyo rais Maduro ambaye ushindi wake katika uchaguzi uliopita wa mwaka 2018 unazingatiwa na mataifa kadhaa ya magharibi kuwa wa udanganyifu, amesema Venezuela inao mfumo wa uwazi katika uchaguzi kuliko taifa jingine lolote duniani. Matokeo ya mwisho yanatarajiwa kutangazwa baadae hii leo.

Vyama vya upinzani vyaungana kuuangusha utawala wa kisoshalisti wa Maduro 

Vyama vya upinzani ambavyo kihistoria vina mipasuko vimeonekana kumuunga mkono mgombea mmoja, na kukipa chama cha Umoja wa Kisoshalisti cha Venezuela ushindani mkubwa kabisa kuwahi kushuhudiwa katika uchaguzi wa rais kwa miongo kadhaa.

Uchaguzi Venezuela
Nyota wa upinzani nchini Venezuela Maria Corina Machado na mgombea wa urais wa upinzani Edmundo Gonzalez.Picha: Ariana Cubillos/AP/picture alliance

Maduro anapingwa na mwanadiplomasia wa zamani Edmundo Gonzalez Urritia, anayeuwakilisha upinzani ulioimarika, na wagombea wengine wanane. 

Hata hivyo jina linalozungumzwa zaidi katika mbio za urais ni Bi Maria Corina Machado. Mbunge huyo wa zamani ameibuka kuwa nyota katika mwaka wa 2023 akijaza pengo lililoachwa wakati kizazi kilichopita cha viongozi wa upinzani kilikimbilia uhamishoni.

Mashambulizi yake dhidi ya ufisadi wa serikali na usimamizi mbaya yaliwahamasisha mamilioni ya Wavenezuela kumpigia kura katika kura za mchujo za upinzani mwezi Oktoba mwaka jana.

Lakini serikali ya Maduro ilizitangaza kura hizo za mchujo kuwa kinyume cha sheria na kufungua uchunguzi wa jinai dhidi ya baadhi ya waandalizi wake.

Tangu wakati huo, imetoa waranti za kukamatwa baadhi ya wafuasi wa Machado na ikawakamata baadhi ya wahudumu wake, na mahakama ya juu ya nchi hiyo ikashikilia uamuzi wa kumfungia kushiriki uchaguzi.

Kwa nini rais Nicolas Maduro anakabiliwa na matatizo?

Venezuela | uchaguzi wa Venezuela
Wafuasi wa rais Nicolas Maduro wa Venezuela.Picha: Cristian Hernandez/AP Photo/picture alliance

Umaarufu wa Maduro umepungua kutokana na mgogoro wa kiuchumi uliosababishwa na kuanguka kwa bei za mafuta, ufisadi na usimamizi mbovu wa serikali.

Maduro anatumai wafuasi wake sugu, wanaofahamika kama Chavistas, wakiwemo mamilioni ya wafanyakazi wa umma na wengine ambao biashara zao au ajira zinategemea serikali. Ndiye mrithi wa Hugo Chavez, msoshalisti maarufu aliyetanua mifumo ya maslahi ya Wavenezuela na kupambana na Marekani.

Maduro alichaguliwa tena mwaka wa 2018, katika kinyang'anyiro kilichozingatiwa na wengi kuwa kiini macho. 

Serikali yake ilipiga marufuku vyama maarufu zaidi vya upinzani Venezuela na wanasiasa dhidi ya kushiriki na, kwa kukosa mazingira sawa ya ushindani, upinzani  ukawahimiza wapiga kura kususia uchaguzi huo.

Zaidi ya Wavenezuela milioni 21 walisajiliwa kupiga kura, lakini kuondoka nchini kwa watu milioni 7.7 kutokana na mzozo ulioendelea kwa muda mrefu, wakiwemo wapiga kura milioni 4, kulitarajiwa kupunguza idadi ya wapiga kura hadi karibu milioni 17.