VFB Stuttgart yapanda katika Bundesliga
18 Februari 2013Wakati ligi za nyumbani wamezidhibiti wakingoja tu kutawazwa mabingwa, Bayern Munich na Barcelona wajitayarisha sasa kunyakua taji la ubingwa wa Champions League.
Tangu mchezo wa 16 wa Bundesliga, VFB Stuttgart ilikuwa tu inaporomoka katika msimamo wa ligi. Ilikuwa wakati huo katika nafasi ya sita, na baada ya kushindwa kuambulia kitu katika michezo mitano mfululizo, ilijikuta katika nafasi ya 15 jana kabla ya kupambana na 1899 Hoffenheim.
Ushindi wa jana wa bao 1-0 dhidi ya Hoffenheim umefikisha mwisho mporomoko huo. Stuttgart sasa imepanda hadi nafasi ya 12 baada ya mchezo wa jana wa 22 katika Bundesliga. Mshambuliaji wa Stuttgart, Vedad Ibisevic, amefarijika na matokeo hayo.
Nayo Hannover 96 ilishindwa kulinda ushindi wake wa mabao 2-1 hadi katika dakika ya 90 ya mchezo wake dhidi ya Nuremberg, na hatimaye katika dakika za majeruhi, Nuremberg ilisawazisha na kuwa sare ya mabao 2-2 katika mchezo wao hapo jana. Christian Schulz mchezaji wa Hannover 96 anasema hakuna la kufanya ila kukubali matokeo.
Bayern Munich imeendeleza ubabe wake katika Bundesliga msimu huu, ambapo hapo siku ya Ijumaa ilifanikiwa kuweka mpira mara mbili katika nyavu za VFL Wolfsburg na kupata ushindi wa mabao 2-0 ugenini.
Borussia Dortmund bado inaifuatilia Bayern japo kwa mbali mno, baada ya ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Eintracht Frankfurt siku ya Jumamosi. Borussia Dortmund ilicheza kwa kipindi kirefu na wachezaji 10 baada ya mshambuliaji wake,Julian Schieber, kutolewa kwa kadi nyekundu katika dakika ya 43 ya kipindi cha kwanza.
Wekeni mambo hadharani
Mkuu wa utawala wa Borussia Dortmund, Hans-Joachim Watzke, amekiri jana kuwa hatarajii mshambuliaji wa timu hiyo kutoka Poland, Robert Lewandowski, kuwa atabakia katika kikosi cha Dortmund msimu ujao na mahasimu wao katika Bundesliga, Bayern Munich wanaonekana kuwa katika nafasi kubwa ya kupata saini ya mchezaji huyo.
"Tumejaribu kila kitu na hata kutoa mafao maalumu kwa kiwango chetu. Lakini iwapo hakiwezi kukubalika unaanza kupata hisia kuwa. mambo hayendi sawa, na kwa sasa siamini kuwa inawezekana Lewandowski kubakia Dortmund", amesema Watzke.
Kocha wa Dortmund, Jurgen Klopp, amekiri kuwa si rahisi kumpata mtu anayeweza kuchukua nafasi ya Lewandowski.
"Iwapo ataondoka, hali ambayo haina uhakika kwa hivi sasa, nadhani tuko tayari kwa hali hiyo," amekiambia kituo cha televisheni cha ZDF.
Edin Dzeko wa Manchester City na Mame Diouf kutoka Senegal mshambuliaji wa Hannover 96 wamewekwa tayari kuchukua nafasi ya Lewandowski katika Dortmund.
Lewandowski mwenye umri wa miaka 24, amefunga mabao 14 msimu huu, wakati mabao yake 30 msimu uliopita yalikuwa ni muhimu kwa Borussia kupata ushindi wa ligi pamoja na kombe la shirikisho na ana mkataba na Dortmund hadi Juni 2014.
Jumamosi wiki hii Watzke amewataka viongozi wa juu wa Bayern kutangaza nia yao hadharani ya kumtaka Lewandowski.
Barani Afrika
Na katika matokeo ya michezo ya kombe la shirikisho barani Afrika, Cofederation Cup, duru ya kwanza jana, LLB Academic ya Burundi iliishinda Polisi ya Rwanda kwa bao 1-0, wakati Power Dynamos ya Zambia iliishinda Recreativo Caala ya Angola lwa bao 1-0. Gor Mahia ya Kenya imetosheka na sare ya bila kufungana na ANSE Reunion ya visiwa vya Sheli sheli, wakati Azam ya Tanzania ikapata ushindi mnono wa mabao 3-1 dhidi ya Al Nassir ya Sudan ya kusini.
Na katika Champions league, Simba ya Tanzania ilikubali kipigo cha bao 1-0 nyumbani dhidi ya FC Libolo ya Angola jana Jumapili.
Champions league barani Ulaya:
Kocha wa Arsenal London Arsene Wenger ameweza kupambana na vipindi kadha vya misukosuko katika kile ambacho ni miaka nane sasa ya kuambulia patupu bila ya taji katika misimu mbali mbali nyumbani , lakini moto unarejea wakati Bayern Munich itakapozuru Uingereza kesho kwa ajili ya pambano la Champions League.
Raia huyo wa Ufaransa , ambaye matatizo yake yameongezeka baada ya timu hiyo kutupwa nje ya vikombe vyaFA na kikosi cha daraja la pili cha Blackburn Rovers siku ya Jumamosi , amekitaka kikisi chake kujitokeza kiume wakati kitakapokumbana na viongozi wa ligi ya Ujerumani Bundesliga katika mpambano wao wa timu 16 bora kesho.
Arsenal walizomewa na mashabiki wao baada ya kuondolewa katika duru ya tano ya kombe la FA na Blackburn, wakikamilisha kuondolewa katika kinyang'anyiro cha kombe mbele ya wapinzani kutoka madaraja ya chini baada ya kuondolewa katika robo fainali ya kombe la ligi na Bradford yadaraja la nne.
Wakati huo huo Malaga ya Uhispania inapaswa kuwa chonjo na masambulizi makubwa dhidi ya Porto ya Ureno hapo kesho katika kinyang'anyiro cha Champions League wakati timu hizo zitakapokutana katika uwanja wa Dragao nchini Ureno.
Mabingwa mara mbili wa Champions League na viongozi wasasa wa ligi nchini Ureno Porto wanashambulia kama nyuki wakiwatumia washambuliaji wao Jackson Martinez kutoka Colombia na James Rodriguez.
Siku ya Jumatano itakuwa zamu wa Barcelona ikitiana kifuani na AC Milan, mpambano ambao utakuwa wa kukata na shoka. Barca imeonyesha umahiri wa hali ya juu nchini Uhispania , wakiongoza kwa points 13 katika kuwania ubingwa wa ligi wakiwa na mabao 48 katika mashindano mbali mbali msimu huu nchini Hispania .
Schalke 04 ina miadi na Galatasaray ya Uturuki, wakati ambapo mshambuliaji nyota katika finali ya Champions league, msimu uliopita Didier Drogba , ambaye ndie aliyefunga bao la mwisho katika mikwaju ya penalti wakati Chelsea ilipokutana na Bayern Munich atakuwa mara hii upande waGalatasaray.
Drogba alipachika bao wakati akianza kuichezea Galatasaray siku ya Ijumaa na atajiunga na mchezaji wa kati kutoka Uholanzi Wesley Sneider wakijaribu kuitupa kando Schalke 04 ya Ujerumani siku ya Jumatano.
Wachezaji wenye hatari kukosa mchezo wa pili
Hata hivyo baadhi yawachezaji wako katika hatari ya kukosa mchezo unaofuata waChampions League iwapo hawatajihadhari katika michezo ya kesho na siku ya Jumatano.
Wachezaji hao ni Laurent Koscielny, na Santi Cazorla wa Arsenal, Dante , Javi Martinez, Bastian Schweinsteiger wote wa Bayern Munich.
Jerome Boateng wa Bayern Munich atakosa mchezo wa kesho.
Abdoulaye Ba wa Porto atakosa mchezo unaofuata iwapo ataonyeshwa kadi ya njano katika mchezo wa kesho, na pia Weligton , na Sergio Sanchez, wote wa Malaga.
Wengine ni Mathieu Flamini, Riccardo Montolivo, daniele Bonera wote waAC Miland, Javier Mascherano, Pedro Rodrigues , Adriano na Alex Song wote wa Barcelona.
Pistorius
Wakati huo huo mwanariadha anayetuhumiwa kumuua mpenzi wake wa kike Oscar pistorius waAfrika kusini amefuta rasmi mbio zote ambazo alikuwa ashiriki katika miezi ijayo kutokana na madai hayo, ameeleza meneja wake jana.
Mwanariadha huyo aliyeshiriki katika mashindano ya olimpiki na wanariadha wenye ulemavu ameshtakiwa siku ya Ijumaa kwa kuuwa kwa kukusudia mpenzi wake mwenye umri wa miaka 29 Reeva Steepkamp , ambaye amepigwa risasi nyumbani kwake mjini Pretoria.
Alipangiwa kushiriki mbio nchini Australia, Brazil, Uingereza na Marekani kati ya Machi na Mei mwaka huu.
Wadhamini na washirika wake wataendelea kuheshimu mikataba walioingia na Pistorius wakisubiri matokeo ya kesi hiyo , ameeleza meneja wake Peet van Zyl .
Mwandishi : Sekione Kitojo / rtre / ape / afpe
Mhariri : Josephat Charo