1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vifo vya Covid-19 vinakaribia milioni 6

7 Machi 2022

Idadi ya vifo duniani vinavyotokana na ugonjwa wa Covid-19 inakaribia kupindukia milioni sita, na kudhihirisha wazi kuwa janga hilo la ulimwengu ambalo linaingia mwaka wake wa tatu bado halijaisha.

https://p.dw.com/p/486xL
Honkong | Patienten warten in Zelt vor dem Krankenhause Caritas Medical Centre
Picha: Liau Chung-ren/ZUMA Wire/imago images

Watu milioni sita kupoteza maisha kutokana na janga la ugonjwa wa Covid-19 ni dhahiri kuwa ugonjwa huo ni hatari licha ya watu kuanza kupuuza masharti ya kudhibiti kusambaa kwa Corona kwa kutovaa barakoa, safari kuanza tena na shughuli nyengine zikirudi kama kawaida kote ulimwengu.

Takwimu rasmi za chuo kikuu cha John Hopkins, Marekani zinaonyesha kuwa kufikia leo Jumatatu, idadi ya watu waliokufa kutokana na ugonjwa wa Covid imefikia 5,999,158.

Soma pia: Maafisa Uganda wapendekeza sheria ya chanjo kuwa lazima

Visiwa vya Pacific, ambavyo kwa zaidi ya miaka miwili vilikuwa vimenusurika na maambukizo ya virusi vya Corona, sasa vinaandamwa na mlipuko na vifo vinavyotokana na aina mpya ya kirusi cha Omicron.

Kadhalika, kisiwa cha kibiashara cha Hong Kong, pia kinashuhudia ongezeko la vifo kutokana na ugonjwa wa Covid-19. Kisiwa hicho chenye idadi ya watu milioni 7.5, sasa kinapima watu wake mara tatu kwa mwezi katika hali ya kujaribu kudhibiti kuenea kwa Corona.

Si hayo tu, katika wakati ambapo vifo vinaendelea kuripotiwa kwa wingi nchini Poland, Hungary, Romania na mataifa mengine ya Ulaya Mashariki, eneo hilo limeshuhudia zaidi ya wakimbizi milioni moja wanaokimbia vita nchini Ukraine, nchi hiyo imekuwa na idadi ndogo ya watu waliopokea chanjo ya Covid-19.

Ama kwa upande wa Marekani, licha ya utajiri wake na upatikanaji rahisi wa chanjo dhidi ya Covid, idadi ya vifo vinavyotokana na Corona katika taifa hilo inakaribia watu milioni moja.

Idadi ya vifo ulimwengu kote inaripotiwa zaidi kwa watu ambao bado hawajapokea chanjo 

Kolumbien Bogota PCR Test
Mwanamke mjini Bogota akifanyiwa vipimo vya CoronaPicha: Chepa Beltran/VWPics/imago images

Tikki Pang, profesa katika chuo kikuu cha Singapore anasema idadi ya vifo ulimwengu kote inaripotiwa zaidi kwa watu ambao bado hawajapokea chanjo dhidi ya virusi hivyo.

Ilichukua muda wa miezi saba kurekodi watu milioni moja wa kwanza waliokufa baada ya ugonjwa wa Covid-19 kutangazwa kuwa janga la ulimwengu mapema mwaka 2020. Miezi minne baadae, watu wengine milioni moja walipoteza Maisha, na tangu wakati huo watu milioni moja wamekuwa wakipoteza maisha kila baada ya miezi mitatu na kufikisha idadi jumla ya watu waliokufa kwa Covid kufikia milioni tano kufikia mwezi Oktoba mwaka jana.

Soma pia: Wananchi wa Rwanda wadai kulazimishwa chanjo ya COVID-19

Sasa idadi hiyo inahofiwa kupindukia milioni sita kote duniani, hiyo ikiwa ni zaidi ya watu wanaoishi katika miji ya Berlin na Brussels ukijumuisha kwa Pamoja au idadi ya watu katika jimbo la Maryland, Marekani.

Idadi hiyo ya milioni sita huenda ikawa kubwa hata Zaidi kutokana na kutokuwepo takwimu kamili za watu waliokufa katika sehemu nyengine duniani miongoni mwa sababu nyengine.

Kwa mujibu wa tathmini iliyofanywa na timu katika jarida la The Economist, wanakadiria kuwa idadi ya vifo vilivyotokana na ugonjwa wa Covid-19 ni kati ya milioni 14 na 23.