1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vifo vya maporomoko ya udongo Uganda vyafikia 20

30 Novemba 2024

Jumuiya ya Msalaba Mwekundu imesema watu 750 wamehamishwa, ambapo 216 kati yao wanaishi kwa muda kwenye shule jirani huku wengine wakihifadhiwa na jamaa zao.

https://p.dw.com/p/4nb4q
Uganda | Maporomoko ya udongo Bulambuli
Wafanyakazi wa Shirika la Msalaba Mwekundu wakisaidia kutafuta watu waliofukiwa na matope.Picha: Nakasiita/AP Photo/picture alliance

Miili zaidi iliyoangukiwa na tope imepatikana mashariki mwa Uganda jana Ijumaa huku mtu mmoja aliyejeruhiwa akifariki hospitalini, na kufanya idadi ya vifo kutokana na maporomoko ya ardhi wiki hii kufikia 20, maafisa wamesema wakati juhudi za utafutaji zikiendelea katika eneo lililoathirika.

Mvua kubwa ilisababisha maporomoko hayo yaliyofunika vijiji sita katika wilaya ya Bulambuli, kilomita 280 mashariki mwa mji mkuu wa Kampala, usiku wa Jumatano. Takriban nyumba 125 ziliharibiwa.

Soma pia: Zaidi ya watu 100 bado wanatafutwa katika maporomoko ya udongo Uganda

Msemaji wa Jumuiya ya Msalaba Mwekundu ya Uganda, Irene Kasiita, aliwaambia wanahabari kuwa miili ya watu wengine wanne ilipatikana siku ya Ijumaa huku mtu wa tano, aliyejeruhiwa kwenye maporomoko hayo, akifariki katika Hospitali ya Mbale.

Jumuiya hiyo ilisema kwenye taarifa kuwa watu 750 walihamishwa, ambapo 216 kati yao wanaishi kwa muda kwenye shule ya jirani huku wengine wakihifadhiwa na ndugu zao.