Vifo vya Tetemeko la Ardhi Afghanistan vyafikia 1,000
22 Juni 2022Afisa wa wizara ya mambo ya ndani ya Afghanistan, Salahuddin Ayubi amesema helikopta zimepelekwa kwa ajili ya kuendeleza juhudi za uokozi na kuwafikia waliojeruhiwa pamoja na kupeleka vifaa vya matibabu na chakula.
Ayubi amesema idadi ya walioathirika inaweza ikaongezeka kutokana na baadhi ya vijiji vilivyopo ndani ndani katika maeneo ya milima na itachukua muda kupata taarifa zaidi.
Ayubi amefafanua kuwa vifo vingi vilivyothibitishwa vimetokea katika jimbo la mashariki la Paktika, ambako watu 255 wameuawa na wengine zaidi ya 200 wamejeruhiwa. Katika jimbo la Khost, watu 25 wameuawa na wengine 90 wamepelekwa hospitali.
Mkurugenzi wa Habari na Utamaduni wa jimbo la Paktika, Mohammad Amin Hozaifa ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba watu 1,000 wamekufa na wengine 1,500 wamejeruhiwa. Kwa mujibu wa Hozaifa, majeruhi wamepelekwa mjini Kabul na Gardez.
Wito wa msaada watolewa kuepusha vifo zaidi
Naibu Waziri wa Afghanistan anayehusika na majanga katika serikali ya Taliban, Mawlawi Sharafuddin Muslim amesema taarifa za awali zinaonesha kuwa wilaya za Gyaa, Neka, Barmal na Zorwaki katika jimbo la Paktika na wilaya ya Speray katika jimbo la Khost na wilaya ya Achin katika jimbo la Nangarhar, watu 920 wamekufa na wengine takriban 610 wamejeruhiwa.
Sharafuddin ameyatolea wito mashirika ya misaada kupeleka wafanyakazi wake mara moja kwenye eneo la tukio ili kuzuia maafa zaidi.
''Tukio kubwa namna hii linapotokea katika nchi, kuna haja ya kupata msaada kutoka nchi nyingine. Ni vigumu sana kwetu kuweza kukabiliana na tukio hili, tunaiomba jumuia ya kimataifa kushirikiana nasi na kuendeleza msaada wao.'' amesema.
Haibatullah Akhundzada, kiongozi mkuu wa kundi la Taliban linalotawala nchini Afghanistan ametuma salamu za rambirambi kufuatia janga hilo. Picha katika vyombo vya habari vya Afghanistan zimeonyesha nyumba zilivyoharibika na miili ikiwa katika vifusi.
Tetemeko hilo ni janga baya zaidi kuwahi kuikumba Afghanistan
Wakati huo huo, shirika la Umoja wa Mataifa linaloratibu misaada ya kiutu, OCHA, limesema linapambana kupata makaazi ya dharura na msaada wa chakula katika eneo na tukio.
Kwa mujibu wa OCHA, washirika wao wa misaada ya kiutu walikuwa wanajiandaa kutoa msaada kwa familia zilizoathirika katika majimbo ya Paktika na Khost, kwa kushirikiana na viongozi wa Taliban.
Shirika la Utafiti wa Jiolojia la Marekani, USGC, limeeleza kuwa tetemeko hilo la leo ni baya zaidi kutokea nchini Afghanistan tangu mwaka 2002 na limepiga umbali wa kilomita 44 kutoka kusini mashariki mwa mji wa Khost, karibu na mpaka wa Pakistan.
Shirika linalohusika na matetemeko ya ardhi barani Ulaya, EMSC limesema kuwa tetemeko hilo la ardhi lilikuwa na ukubwa wa 6.1 katika kipimo cha Richta, huku USGC, ikisema lilikuwa na ukubwa wa 5.9 katika kipimo cha Richta.
Mwezi Januari, tetemeko la ardhi lilitokea magharibi mwa Afghanistan na kuwaua zaidi ya watu 20.