Vijana wa Afrika wazitaka serikali kuunga mkono uvumbuzi wao
5 Juni 2019Vijana hao wamesema, kwa mtazamo wao, wataweza kuchangia zaidi katika kuimarisha maisha ya jamii pamoja na kuokoa kiasi kikubwa cha fedha zinazotumiwa kuagiza vifaa mbadala ya vile wanavyovumbua. Kwa namna hiyo watashiriki moja kwa moja katika kutatua changamoto za kila siku maishani mwa watu wa Afrika.
Mhandisi Neo Hutiri kutoka Afrika Kusini ameibuka mshindi wa mwaka huu wa tuzo ya uvumbuzi katika Uhandisi inayodhaminiwa na taasisi ya uhandisi ya ufalme wa Uingereza. Washindi wengine wa tuzo hiyo inayoandamana na fedha taslimu zipatazo (pauni elfu 55) za Uingereza wametokea Nigeria, Uganda na Kenya.
Fainali hizo zilifanyika jana 04.05.2019 mjini Kampala na kuhudhuriwa na wavumbuzi, wataalamu na wanafunzi wa uhandisi kutoka sehemu mbalimbali za Afrika waliokuja kushiriki au kushuhudia kilele cha tuzo hiyo. Vijana wavumbuzi wametoa mwito kwa serikali za bara Afrika nazo zidhihirishe kwamba zinathamini kazi za vijana kwa kuwekeza pia katika mashindano kama hayo.
Mshindi wa mwaka jana Ashraf Sekito Kutoka Uganda alivumbua kifaa kijulikanacho kama ‘matibabu' ambacho kinaweza kupima ugonjwa wa malaria kwa wepesi na kwa gharama ndogo. Lakini hadi sasa serikali ya Uganda haijaanza kutumia mbinu hiyo wala kuonyesha kwamba iko tayari kumsaidia kutengeneza vifaa hivyo kwa wingi.
Kinyume na Ashraf, mshindi wa mwaka huu Neo Hutiri ameelezea kuwa serikali ya Afrika Kusini imeanza kutumia uvumbuzi wake ujulikanao kama Pelebox katika kuwezesha wanaougua magonjwa sugu kupata dawa zao kwa wepesi. Mshindi mwingine wa mwaka huu ni Roy Allela kutoka Kenya aliyevumbua glavu zinazoweza kutumiwa katika kutafsiri lugha ya ishara chini ya mfumo wake ujulikanao kama Sign-IO
Washiriki 16 waliweza kufika kwenye ngazi ya fainali za mwaka huu ambapo mshindi wa kwanza amepokea pauni 25,000 za Uingereza na waliofuata katika nafasi tatu wakapokea 10,000 kila mmoja.