1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vikosi vya kimataifa kupelekwa Mali

21 Desemba 2012

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeidhinisha kwa kauli moja azimio la kupeleka kikosi cha jeshi Mali, kitakachoongozwa na Afrika ili kupambana na wapiganaji wenye itikadi kali za Kiislamu kaskazini mwa nchi hiyo.

https://p.dw.com/p/177L9
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa
Baraza la Usalama la Umoja wa MataifaPicha: dapd

Azimio hilo lililopitishwa na wanachama wote 15 wa baraza hilo la Umoja wa Mataifa limekipa mamlaka ya mwaka mmoja kikosi hicho kinachojulikana kama AFISMA, kuisaidia serikali ya Mali kupambana na makundi yenye silaha nchini humo. Lakini baraza hilo limesema kikosi hicho cha kijeshi kitaanza operesheni zake baada ya Mali kupiga hatua katika juhudi za kisiasa na hali ya kuleta maridhiano na limesisitiza kuwa mipango ya kijeshi itapitiwa upya na kuidhinishwa kabla ya kuanza kwa operesheni zozote.

ECOWAS ina wanajeshi 3,300

Jumuiya ya Kiuchumi ya Mataifa ya Afrika Magharibi-ECOWAS, imesema ina wanajeshi 3,300 ambao wako tayari kwenda nchini Mali kwa lengo la kusaidia operesheni za kijeshi, mpango ambao waratibu wanasema hauwezi kuanza kabla ya mwezi Septemba mwaka ujao. Waasi wa Tuareg na makundi mengine yenye itikadi kali za Kiislamu yamelidhibiti eneo la Kaskazini mwa Mali tangu mwezi Machi mwaka huu baada ya kufanyika mapinduzi ya kijeshi nchini humo.

Viongozi wa ECOWAS
Viongozi wa ECOWASPicha: PIUS UTOMI EKPEI/AFP/Getty Images

Waziri wa Mambo ya Nje wa Mali, Tieman Coulibaly amelipokea kwa furaha azimio hilo na amesema hiyo ni hatua moja mbele ya kihistoria katika kupambana na makundi yenye mafungamano na mtandao wa kigaidi wa Al-Qaeda. Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon, ECOWAS, Umoja wa Afrika na mataifa mengine yanayohusika na suala la Mali yanapaswa kuhakikisha kuwa baraza hilo linaridhishwa na mipango hiyo ya operesheni za kijeshi nchini Mali.

Ufaransa na Marekani tayari zinafanya kazi na jeshi la Mali. Azimio hilo linataka mchakato wa kisiasa ufanyike kwa haraka ili waasi wa Tuareg waingizwe katika muungano wa kupambana na makundi ya wapiganaji. Azimio hilo linataka kuboreshwa kwa mipango ya kijeshi na kuwekwa mikakati na malengo ya kupiga hatua za kisiasa na maandalizi ya kikosi hicho. Balozi wa Ufaransa kwenye Umoja wa Mataifa, Gerard Araud amesema hakuna mtu anayepuuzia majukumu yanayoisubiri jumuiya ya kimataifa ya kumaliza vitendo vya kigaidi kaskazini mwa Mali.

Kundi mojawapo linalodhibiti kaskazini mwa Mali
Kundi mojawapo linalodhibiti kaskazini mwa MaliPicha: Reuters

Suala la fedha lawa tete

Suala la fedha limekuwa lenye utata hata kabla ya kuidhinishwa kwa kikosi hicho. Ban Ki-Moon aliyakasirisha mataifa ya Afrika pale aliposema kuwa Umoja wa Mataifa hauwezi kukifadhili kikosi hicho. Wanadiplomasia wanasema kuwa sasa Ban yuko katika shinikizo la kutafuta njia za kukipatia fedha kikosi hicho kwa ajili ya msaada wa kiufundi. Azimio hilo linazitaka nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa na mashirika ya kimataifa kutoa fedha kwa ajili ya AFISMA. Baraza la Usalama la umoja huo limesema linafikiria kuanzisha mfuko mpya wa fedha wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya kununua vifaa na huduma mbalimbali za wanajeshi. Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, hadi sasa mzozo wa kaskazini mwa Mali umesababisha zaidi ya watu 400,000 kuyakimbia makaazi yao.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/ AFPE
Mhariri: Daniel Gakuba