1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vikosi vya Rwanda vyafanya vema Msumbiji

Saleh Mwanamilongo
30 Julai 2021

Jeshi la Rwanda lililopelekwa Cabo Delgado nchini Msumbiji limetangaza kufanya vyema kwenye uwanja wa mapigano huku kukiwa na wasiwasi kuhusu kamanda wa kikosi hicho.

https://p.dw.com/p/3yKuF
Symbolbild I Militär Ruanda
Picha: Jean Bizimana/REUTERS

Msemaji wa jeshi la Rwanda ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba wanamgambo 14 wameuliwa wiki hii na wanajeshi kutoka Rwanda waliopelekwa Msumbiji.

Ronald Rwivanga amesema operesheni za kijeshi zilizoendeshwa kwenye maeneo ya Mbau na Awese,mkoani Cabo Delgado, baada ya kikosi cha wanajeshi wake kuvamiwa, zilisababisha jumla ya wanamgambo 14 kuuliwa. Rwivanga amesema ni majeraha madogo yaliowapata wanajeshi wa Rwanda kufuatia operesheni hizo.

Kuhifadhi maslahi ya raia wa Msumbiji ?

Mapema mwezi huu, Rwanda ilipeleka kikosi cha wanajeshi na polisi 1,000 nchini Msumbiji kusaidia katika kupamabana na kundi la waasi linaloendesha mashambulizi kaskazini mwa nchi hiyo.  Takriban raia laki nane waliyahama makaazi yao kwenye mkoa wa Cabo Delgado na mapigano hayo yalisababisha kampuni ya Mafuta ya Ufaransa ya Total kusitisha mradi wake wa dola bilioni 20 wa kuzalisha gesi asilia kwenye mkoa huo.

 Ikiwa kupelekwa kwa kikosi cha wanajeshi wa Rwanda nchini Msumbiji kunalenga kuwasaka wanamgambo wenye itikali kali. Lakini wakosoaji wa serikali ya Rwanda wanaoishi nchini humo wanahofia usalama wao pia. Jenerali Innoncent Kabandana anayeongoza kikosi hicho, ameelezwa na wapinzani kuwa ni mkono wa rais Paul Kagame katika kuwalenga wakosoaji wake.

Hofu ya wakimbizi wa Rwanda

Symbolbild I Militär Ruanda
Picha: Jean Bizimana/REUTERS

 Mtandao wa TheRwandan.com, uliandaka kuwa Meja-jenerali Kabandana alihusika na mauwaji ya maaskofu wa kanisa katoliki wa Gakurazo mwaka 1994 nchini Rwanda na vilevile kuwalenga wakosoaji wa serikali ya Rwanda nchini Marekani na Canada ambako alifanya kazi kama mwambata wa kijeshi katika ubalozi wa Rwanda jijini Washington.

Cleophas Habiyareme, mkuu wa jamii ya wakimbizi wa Rwanda wanaoishi nchini Msumbiji amesema alisoma taarifa pia kwamba kamanda huyo anahusika na kuwalenga wapinzani wanaoishi nje ya nchi. Lakini amesema hilo haliwezi kuwatisha jamii ya wakimbizi wa Rwanda nchini Msumbiji. Habiyareme amesema Msumbiji ni nchi iliyosaini mkataba wa Geneva kwa jili ya kuwapa hifadhi wakimbizi. Amesema halitokuwa jambo la busara kwa kikosi kilicho alikwa kwa shughuli malumu baadae kuanza kuwalenga wakimbizi. Hata hivyo ameiomba serikali ya Msumbiji kuhakikisha usalama wao.

Nchini Msumbiji ambako jenerali Kabandana amepewa majukumu mapya, jamii ya wakimzizi wa Rwanda  ni takriban watu 4,000 ambao wamekuwa wakibughudhiwa na kuuliwa miaka ya hivi karibuni.  Kisa cha hivi karibuni ni kutoweka bila maelezo yoyote hadi sasa kwa mwandishi habari na mkosoaji wa serikali ya Rwanda Ntamuhanga Cassien aliyekuwa akiishi kwenye kisiwa cha Inhaca,nchini Msumbiji.