Vikosi vya Syria vyapelekwa Manbij
28 Desemba 2018Hatua hiyo imekuja kutokana na kitisho cha mashambulizi kutoka majeshi ya Uturuki huku nchi hiyo ikipinga hatua hiyo iliyochukuliwa na wanamgambo hao.
Uturuki imesema leo kwamba wanamgambo wa Kikurdi nchini Syria hawana haki ya kuomba msaada kutoka serikali ya Syria kupambana na kitisho hicho cha mashambulizi kutoka Uturuki upande wa kaskazini.
Wanamgambo wa kundi lijiitallo Vikosi vya Ulinzi wa Umma, YPG, vinavyodhibiti eneo hilo kwa silaha hawana haki ama nguvu za kutoa taarifa ya kukaribisha makundi mengine kwa niaba ya watu wa eneo hilo, imesema wizara ya ulinzi ya Uturuki.
Vikosi vya serikali ya Syria vilivyopelekwa katika eneo la Manbij vimeingia katika mji wa Manbij kwa mujibu wa msemaji wa jeshi la Syria brigedia jenerali Ali Mayhoub.
"Taarifa ya mamlaka kuu ya jeshi la Syria, kwa misingi ya jeshi la ulinzi na dhamira yake ya jumla kuhusiana na jukumu la utekelezaji wa ulinzi wa kila sehemu ya mipaka ya jamhuri ya Syria, na kujibu miito ya watu wa Manbij, majeshi ya ulinzi yametangaza kwamba wapiganaji wa jeshi ya Syria wameingia Manbij na kupandisha bendera ya jamhuri ya Kiarabu ya Syria."
Syria yapeleka majeshi Manbij
Shirika linaloangalia haki za binadamu nchini Syria, lenye makao yake makuu nchini Uingereza, limesema majeshi ya serikali yamewekwa nje ya mji huo, kati ya mji huo na eneo ambalo liko katika ushawishi wa Uturuki.
Uamuzi wa ghafla wa rais wa Marekani Donald Trump kuviondoa vikosi vya jeshi la nchi hiyo kutoka Syria kumewatia shaka wapiganaji wanaoongozwa na Wakurdi ambao wamepambana na kundi linalojiita dola la Kiislamu pamoja nao kwa miaka kadhaa.
Viongozi wa Wakurdi wanahangaika kupata mkakati wa kule kulilinda jimbo lao ambalo limesambaa katika maeneo ya kaskazini na mashariki, ambako kuwapo kwa wanajeshi 2,000 wa Marekani kumezuwia hadi sasa mashambulizi ya Uturuki, ambayo inawaangalia wapiganaji wa Kikurdi kuwa kitisho kwa maeneo yao na imeapa kuwamaliza.
Mji huo unashikilwa na baraza la kijeshi la manbij, wapiganaji wenye mafungamano na kundi la jeshi la Syria, wanapakana na maeneo yanayoshikiliwa na waasi wanaoungwa mkono na Uturuki ambao wamekuwa wakijitayarisha kwa mashabulizi.
Mwandishi: Sekione Kitojo/rtre
Mhariri: Mohammed Khelef