Vikwazo vya silaha havisaidii kuzuia biashara haramu ya silaha ndogo ndogo
12 Septemba 2007Uchunguzi mpya wa Umoja wa Mataifa juu ya biashara haramu ya silaha ndogo ndogo unaomnukulu Nicholas Cage, unasema ingawa matamshi yake ni ya kibeuzi yanadhihirisha kuongezeka kwa tatizo la biashara haramu ya silaha hizo. Katika filamu ya Lord of War, Cage anamwambia kiongozi wa kundi la waasi linalotaka silaha haramu na hapa nanukulu, ´Ikiwa nitafanya kazi yangu vizuri, kikwazo cha silaha kinatakiwa kuwa vigumu kutekeleza, mwisho wa kumnukulu Cage, mchezaji filamu wa Hollywood.
Nicholas Cage, anayecheza nafasi ya mfanyabiashara wa silaha katika filamu ya mwaka wa 2005 iitwayo ´Lord of War´, anapuuza vikwazo vya silaha. Anasema aidha viwe vimewekwa na Marekani au Umoja wa Mataifa, vikwazo vya silaha hufaulu kwa kiwango kidogo sana au hata viwe havina maana yoyote katika kuzuia biashara haramu ya silaha.
Ripoti ya kurasa 26 itakayowasilishwa katika mkutano ujao wa baraza kuu la Umoja wa Mataifa kuanzia tarehe 18 mwezi huu, inadokeza kuwa biashara ya silaha inafanywa kupitia mipango ya usafiri ambayo njia zake hazieleweki na ulipaji wa fedha usioweza kugunduliwa.
Lakini shughuli hizo za biashara haramu ya silaha zimesababisha athari kubwa na zimekuwa sababu muhimu ya kuvunja vikwazo vya silaha vilivyowekwa na baraza la usalama la Umoja wa Mataifa. Kutumia stakabadhi za uongo na vyeti bandia, wafanyabiashara wa silaha wamefaulu kukiuka vikwazo katika nchi kadhaa za Afrika ikiwa ni pamoja na Angola, Ivory Coast, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, Liberia, Sierra Leone, Somalia na Sudan.
Ukiukaji huo wa vikwazo unafanywa na mitandao ya kimataifa ya washenga wanaojihusisha na biashara haramu ya silaha. Kufikia katikati ya mwaka huu takriban nchi 40 zilikuwa zimetekeleza sheria za kitaifa na taratibu dhidi ya biashara ya silaha. Idadi hiyo bado ni ndogo mno ikizingatiwa kwamba Umoja wa Mataifa una nchi 192 wanachama.
Matokeo yake ni kuwa mwanya wa kuingizia silaha katika nchi nyingi ni mkubwa kiasi cha kuziwezesha ndege kubwa kusafirisha shehena za bunduki aina ya AK 47, mojawapo ya silaha zinazotumiwa sana katika maeneo ya upinzani duniani kote.
Wakati Mikhail Kalashnikov, mrusi aliyeitengeneza bunduki ya AK 47, yaani Automatic Kalashnikov, mnamo mwaka wa 1947, alipoulizwa ikiwa alikuwa na matatizo ya kulala usiku akiota ndoto za kuogofya kuhusu mamia na maelfu ya watu wanaouwawa kutumia bunduki yake, alisema na hapa namnukulu, ´Nalala vizuri. Ni wanasiasa ndio wanaotakiwa kulaumiwa kwa sababu wanashindwa kukubaliana na badala yake wanageukia kusuluhisha matatizo yao kupitia machafuko,´ mwisho wa kumunukulu mrusi huyo Mikhail Kalashnikov.
Daniel Prins, mwenyekiti wa kundi la watalaamu wa serikali mbalimbali anasema utafiti umeonyesha kuwa wafanyabiashra wa silaha wana jukumu kubwa katika kuendeleza biashara haramu ya silaha ndogo ndogo na kuenea kwa upatikanaji wa silaha hizo. Kwa kuwa silaha ndogo zinachukuliwa kuwa silaha zinazotumiwa sana katika maeneo ya machafuko na harakati ndogo za kijeshi duniani, zimeelezwa kuwa silaha halisi za maangamizo na wala sio nuklia, wala silaha za kibayolojia au kemikali.
Balozi wa Sri Lanka, Prasad Kariyawasam, aliyekuwa mwenyekiti wa mkutano wa mwaka jana wa Umoja wa Mataifa kuhusu silaha ndogo ndogo amesema kuweka vikwazo vya silaha hutatua tu sehemu ndogo ya tatizo zima la biashara haramu ya silaha kwa sababu hakuzishughulikii kabisa sababu halisi za tatizo hilo.
Balozi Kariyawasam ameongeza kusema kwamba vikwazo vya silaha huzingatia tu upande unaohitaji silaha na wala sio upande unaouza. Katika biashara ya dawa za kulevya, sheria za kimataifa zinatuwama upande unaouza hivyo ipo haja ya kuongeza juhudi kuzingatia zaidi upande wa wauzaji silaha katika biashara haramu ya silaha. Kiongozi huyo amesema ipo haja ya kuzishungulikia pande zote husika kwa viwango sawa ili kuzuia utapakazaji wa silaha ndogo ndogo.
Ripoti ya uchunguzi wa Umoja wa Mataifa pia inasema wafanyabiashara haramu wanaofanya kazi katika mazingira mbalimbali ulimwenguni kote mara kwa mara hawamiliki bidhaa wanazozishughulikia bali hutumia ongezeko la fursa katika usafirishaji wa kimataifa, fedha na mawasiliano.