Vilabu vya Bundesliga vyaidhinisha hatua za usalama
14 Desemba 2012Mapendekezo hayo ni pamoja na kuwakagua vilivyo mashabiki katika michuano mikubwa, kuondoa kabisa matumizi ya fataki ambazo tayari zimepigwa marufuku na kuwapa adhabu kali kwa wale watakaokiuka sheria hizo.
Sheria hizo zimezusha tetesi kutoka baadhi ya makundi ya mashabiki yenye wasiwasi kwamba vilabu vinalenga hasa kuondoa utamaduni maarufu wa masbahiki kusimama viwanjani katika soka ya vilabu Ujerumani. Hata Hivyo maafisa wa Ligi wamekanusha madai hayo.
Huub Stevesn ahakikishwia kazi yake
Kwingineko Mkufunzi wa klabu ya Schalke 04 Huub Stevens amehakikishiwa kuwa atasalia katika uongozi wa klabu hiyo ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, hata baada ya mchuano wa mwisho mwaka huu dhidi ya Freiburg leo Jumamosi, na licha ya matokeo duni katika mechi za karibuni.
Mkurugenzi wa michezo wa klabu Horst Heldt amesema klabu hiyo itaendelea kuwa na utulivu wakati ikijadili masuala hayo yote. Heldt amesema mambo yatakuwa mazuri tena na wataanza kusjaili ushindi. Schalke wamepoteza mechi zake tatu za mwisho na hawajashinda hata moja kati ya mechi tano na kusonga nafasi ya tano katika Bundesliga.
Schalke ambao pia wako katika kinyang'anyiro cha kombe la shirikisho wiki ijayo, wamefuzu katika awamu ya 16 ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa kumaliza wa kwanza katika kundi lao. Wakati huo huo, kiungo wa Schalke Jermaine Jones amepigwa marufuku kushiri mechi nne za Bundesliga baada ya kufurushwa uwanjani katika mchuano wa wiki iliyopita walioshioshindwa magoli matatu kwa moja na Stuttgart. Jones anashikilia rekodi ya klabu hiyo kwa kufurushwa uwanjani mara tano.
Löw aridhika na matokeo ya vilabu vya Bundesliga
Mkufunzi wa timu ya kandanda ya Ujerumani maarufu kama Die Mannshaft Joachim Löw amesema rekodi ya timu saba za Bundesliga kufuzu katika awamu ya mwondowano katika Champions League na Europa League, inapaswa kuisaidia timu ya taifa ya Ujerumani kupata mafanikio barani Ulaya. Löw amesema yamekuwa matarajio yake kwamba Ujerumani iwe na timu nyingi katika awamu ya mwondowano na siyo Bayern pekee. Amesema ni muhimu kwa wachezaji kupata ujuzi, na kutengeneza msingi imara kwa mwaka ujao.
Kwa mara ya kwanza vilabu saba vya Ujerumani vitashiriki katika awamu ya mwondowano katika Ligi ya Mabingwa na pia Europa, wakati droo itakapofanywa katika makao makuu ya Shirikisho la Soka Ulaya UEFA mjini Nyon, Uswisi mnamo Desemba 20. Bayern Munich, Borussia Dortmund na Schalke 04 viko katika Ligi ya Mabingwa wakati Bayer Leverkusen, Hanover 96, VFB Stuttgart na Borussia Moenchengladbach vikishiriki katika awamu ya 32 ya Ligi ya Europa.
Ujerumani wako kileleni mwa kundi lao la kufuzu katika dimba la dunia mwaka wa 2014 nchini Brazil na uongozi wa tofauti ya pointi tatu mbele ya nambari mbili Sweden ambao hawajacheza mchuano mmoja. Ujerumani inacheza mchuano wake wa kwanza wa kimataifa mwaka wa 2013 dhidi ya Ufaransa mjini Paris mnamo Februari sita katika mchuano wa kirafiki, kasha wapambane na Kazakhstan nyumbani na ugenini katika mechi za kufuzu kwa dimba la dunia mwezi Machi.
Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA/Reuters
Mhariri: Josephat Charo