Viongozi 40 wa Belarus kuwekewa vikwazo na Umoja wa Ulaya
2 Oktoba 2020Viongozi wa Umoja wa Ulaya mapema leo wamekubaliana kuwawekea vikwazo maafisa wa Belarus, na kumaliza mkwamo na Cyprus iliyokuwa ikizuia kutekelezwa kwa hatua hiyo baada ya umoja huo kukubali kuitumia onyo kali Uturuki.
Vikwazo hivyo vinawalenga maafisa 40 wa Belarus, kwa kughushi uchaguzi pamoja na kuwakandamiza waandamanaji walioingia mitaani kupinga matokeo ya uchaguzi wa Agosti 9 uliompa ushindi Rais wa Belarus Alexander Lukashenko.
Soma zaidi: Maelfu waandamana tena huko Belarus dhidi ya Lukashenko
Lukashenko alichaguliwa tena kwa muhula wa sita madarakani kwa ushindi wa asilimia 80 ya kura zote zilizopigwa. Lukashenko ameshikilia wadhifa huo tangu mwaka1994.
Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya Charles Michel amewaambia waandishi habari ni muhimu sana kutekeleza uamuzi wao walioufikia wiki kadhaa zilizopita, na kutoa ishara kuwa umoja wao ni wa kuaminika.
Lukashenko hakuwekwa kwenye orodha hiyo ya vikwazo, ingawa Michel amesema huenda orodha hiyo ikafanyiwa mabadiliko kadri Umoja wa Ulaya unavyoendelea kufuatilia hali inavyoendelea nchini Belarus.
"Kuhusu Lukashenko: hapana, Lukashenko hayumo kwenye orodha ya sasa. Lakini kwa kweli tutafuatilia hali inavyoendelea. Tungependa kuona mazungumzo ya pamoja Belarusi," amesema Michel.
Lukashenko huenda akawekewa vikwazo
Wanadiplomasia wa umoja huo wamesema kiongozi huyo huenda naye akawekewa vikwazo siku za usoni, iwapo atakataa kufanya mazungumzo na upande wa upinzani.
Sio jambo la kawaida kwamba nchi zote 27 wanachama wa Umoja wa Ulaya, zimeyakataa matokeo ya uchaguzi wa Agosti 9 yaliomrejesha Lukashenko madarakani kwa kipindi cha miaka sita. Wote wanataka uchaguzi mpya.
Soma zaidi: Lukashenko hana dalili ya kuondoka madarakani huko Belarus
Hatua dhidi ya maafisa wa Belarusi zilikubaliwa mnamo mwezi Agosti lakini zilishindikana kutekelezwa kutokana na msimamo wa Cyprus ambayo aliuhimiza Umoja wa Ulaya kuchukua hatua kali dhidi ya Uturuki juu ya shughuli zake za kuchimba gesi mashariki mwa Mediterania.
Uturuki inadaiwa kuchimba gesi hiyo katika maeneo yaliyo karibu na Cyprus pamoja na Ugiriki. Lakini inakana madai hayo na kusema kuwa inafanya operesheni hiyo katika eneo lake.
Maswala haya mawili hayahusiani moja kwa moja, lakini Cyprus ilisema Umoja wa Ulaya lazima uoneshe usawa katika kushughulikia ukiukaji wa kanuni za msingi.
Vyanzo: (dpa,ap,dw)