1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaBrazil

Uvamizi wa majengo ya utawala Brazil walaaniwa

9 Januari 2023

Viongozi wa mataifa kadhaa duniani wamelaani uvamizi wa majengo ya utawala nchini Brazil uliofanywa na wafuasi wa rais zamani wa nchi hiyo Jair Bolsonaro ambao wanapinga matokeo ya uchaguzi uliopita.

https://p.dw.com/p/4Lt1q
Brasilien Brasilia | Bolsonaro Anhänger stürmen Palácio do Planalto
Picha: Ueslei Marcelino/REUTERS

Mkasa huo wa siku ya Jumapili umezusha ukosoaji mkubwa kutoka kwa viongozi wa mataifa chungunzima tangu yale ya  Amerika ya Kusini, Amerika ya Kaskazini na barani Ulaya.

Wengi wameelezea kufadhaishwa na vurumai iliyotokea jana mjini Brazilia, ambako wafuasi wa rais aliyeondoka madarakani nchini Brazil Jair Bolsonaro waliyavamia majengo ya Bunge, Mahakama ya Juu na makaazi ya rais kupinga utawala mpya wa  mwanasiasa wa mrengo wa shoto Luiz Inacio Lula da Silva aliyeapishwa wiki moja iliyopita kuliongoza taifa hilo.

Rais Joe Biden wa Marekani amekitaja kisa hicho kuwa "maudhi" akisema serikali mjini Washington inaalani vikali shambulio hilo dhidi ya demokrasia na kwamba inamuunga mkono rais Lula.

Kiongozi wa Mexico Andres Manuel Lopez Obrador aliandika kupitia ukurasa wa Twitter kwamba "Lula hayuko peke yake" na anaungwa mkono na wana mageuzi nchini mwake, nchini Mexico na eneo zima la Amerika.

Ujumbe sawa nao huo ulitolewa pia na viongozi wa Argentina, Colombia, Bolivia, Cuba na Venezuela. Rais wa Chile Gabriel Boric ameutaja uvamizi huo kuwa shambulizi la woga dhidi ya demokrasia na kutumia ujumbe wake kumkikishia rais Lula kuwa serikali mjini Santiago inamuunga mkono kikamilifu.

Macron na Umoja wa Ulaya walaani "vitimbi" mjini Brazilia 

Brasilien Brasilia | Bolsonaro Anhänger stürmen Palácio do Planalto
Picha: Eraldo Peres/AP Photo/picture alliance

Barani Ulaya, rais Emmanuel Macron wa Ufaransa alituma ujumbe wa kumuunga mkono rais Lula na kuongeza kwamba taasisi za kidemokrasia ni lazima ziheshime.

Kwa upande wake Umoja wa Ulaya kupitia mwanadiplomasia wake mkuu Joseph Borell  umesema umeshtushwa na matendo ya vurugu yaliyofanywa na waandamanaji dhidi ya majengo ya serikali mjini Brazilia na kuongeza kwamba demokrasia ya Brazil itashamiri licha ya "vitimbi vya wafanya vurugu na wenye misimamo mikali."

Katika mkasa huo wa jana maelfu ya waandamanaji wanaokataa kuyatambua matokeo ya uchaguzi wa mwezi Oktoba yaliyompa ushindi Lula, walivuka vizuizi vya usalama, wakaparamia kuta za majengo na kisha kuyavamia majengo matatu ya utawala yanayopatikana eneo moja katika mji mkuu wa Brazil, Brazilia.

Polisi ilitumia mabomu ya machozi kujaribu kuwadhibiti waandamanaji ambao baadhi walitoa mwito kwa jeshi kuingilia kati ili kumrejesha Bolsonaro madarakani.

Baada ya mshike mshike wa saa kadhaa maafisa wa usalama walisema wamefanikiwa kurejesha udhibiti wa majengo hayo na mamia ya waandamanaji wamekamatwa.

Rais Lula: Wote waliohusika watakamatwa na kuadhibiwa 

Brasilien Brasilia | Bolsonaro Anhänger stürmen Palácio do Planalto
Picha: Eraldo Peres/AP Photo/picture alliance

Rais Lula mwenyewe akizungumza saa chache baada ya mkasa huo amewataja wale waliohusika kuwa "mafashisti" na ameapa kuwasaka na kuwaadhibu.

"Na ninataka kuwaambia kwamba watu wote waliofanya hayo watapatikana na kuadhibiwa. Watatanaba´hi kuwa demokrasia inatoa hakikisho la haki ya uhuru, uhuru wa mawasiliano, uhuru wa kujieleza lakini inahitaji pia watu waheshimu taasisi zilizoundwa kuimarisha demokrasia" amesema kiongozi huyo

Saa chache zilizopita rais wa zamani wa Brazil Jair Bolsonaro amejitokeza kulaani kisa hicho huku akiyapinga madai yanayomhusisha kuyachochea. Bolsonaro alitoa ujumbe huo kupitia mtandao wa Twitter muda mfupi baada ya chama chake kiitwacho Liberal Party kulaani uvamizi uliofanywa na wafuasi wake.

Chama hicho kimesema matukio yaliyoshuhuiwa mjini Brazilia yanafedhehesha, lakini hayawakilishi mtazamo wa chama cha LP wala Bolsonaro na kwamba chama hicho kinaheshimu demokrasia.