Viongozi kuhudhuria ibada ya mazishi ya Castro
29 Novemba 2016Hata hivyo Rais wa Marekani Barack Obama na viongozi kadhaa wa Ulaya hawatahudhuria ibada hiyo. Marekani haijatangaza ni nani atakayeongoza ujumbe wake huku Canada ambayo Waziri Mkuu wake Justin Trudeau aliyeshutumiwa kwa kumtaja Castro kama kiongozi wa kipekee itawakilishiwa na Gavana David Johnston.
Kansela wa zamani wa Ujerumani Gerhard Schroeder atamwakilisha Kansela Angela Merkel katika ibada hiyo inayofanyika katika ukumbi wa mapinduzi mjini Havana. Waziri mkuu wa Ugiriki Alexis Tsipras ndiye kiongozi pekee wa Ulaya aliyethibitisha kuhudhuria.
Viongozi wa Afrika wamtaja Castro shujaa
Rais wa Zimbabwe Robert Mugabe, wa Guinea ya Ikweta Teodoro Obiang Nguema, Wa Afrika Kusini Jacob Zuma na Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta watahudhuria ibada hiyo ya mazishi. Cuba ilitangaza siku tisa za maombolezi. Viongozi wa nchi za Amerika ya Kusini akiwemo Rais wa Venezuela Nicolas Maduro na wa Bolivia Evo Morales wanahudhuria ibada hiyo.
Fidel Castro ambaye baadhi wanamtizama kama muasi na wengine kumuona shujaa alinyakua madaraka mwaka 1959 na kuliongoza taifa la Cuba kwa nusu karne. Kutokana na hali mbaya ya afya, alilazimika kumkabidhi madaraka ndugu yake Raul Castro mwaka 2008.
Kwa wengi katika nchi za Amerika ya Kusini na za Afrika, Castro ni ishara ya shujaa aliyepinga ubeberu, kwa kumng'oa madarakani kiongozi dikteta aliyekuwa anaungwa mkono na Marekani na mtetezi wa masikini.
Kuna wanaomuenzi na wanaoshutumu
Hata hivyo wengine wanamshutumu kwa kuwa dikteta ambaye sera zake za ujamaa zinalumiwa kwa kuuharibu uchumi wa Cuba. Korea Kaskazini iliyosema kuwa imempoteza mshirika wake mkubwa dhidi ya Marekani imetangaza siku tatu za maombolezi.
Kulingana na vyombo vya habari vya Japan mara ya mwisho Korea Kaskazini kumuomboleza kiongozi wa nchi za kigeni kwa namna hiyo ni wakati kiongozi wa Palestina Yassser Arafat alipofariki dunia mwaka 2004.
Shule zote na ofisi za serikali zitafungwa leo ili Wacuba waweze kuhudhuria mkutano huo wa hadhara na shughuli nyingine za kutoa heshima za mwisho kwa kiongozi wao. Waombolezaji pia walikuwa wakiweka saini za kiapo kuahidi kutekeleza uzalendo na pia kutii kanuni za ujamaa.
Kuanzia hapo kesho, majivu ya mwili wake utakaotekezwa yatatembezwa katika nchi hiyo kwa kupita katika vituo vyote alikofanya safari yake ya mapinduzi. Siku ya Jumapili, majivu hayo yatazikwa katika mji wa Santiago.
Mwandishi: Caro Robi/afp/Reuters/AP
Mhariri: Bruce Amani