Viongozi na wadau wa Bundesliga kujadili hatima ya msimu huu
16 Machi 2020Viongozi wa Bundesliga walikuwa wanatafakari kufanya maamuzi makali kabla ya mkutano wao leo mjini Frnkfurt ambao unatarajiwa kuthibitisha kusitishwa kwa michezo hadi mapema mwezi ujao. Rais wa heshima wa Bayern Munich Uli Hoeness amesema "Hakuna muongozo maalum" wa namna gani ya kufanya kupambana na dharura hii ya kuzuka kwa virusi vya Corona na kutoa wito kwa wapenzi wa kandanda kuwa wavumilivu.
Hatimaye tunapaswa kukubali hali halisi. Inatubidi kusubiri kwa wiki nne, na kuanza upya kabisa. Huenda tunapaswa kusitisha kucheza kandanda mwezi Oktoba," amesema katika televisheni ya Sport 1. Wadau wa ligi wanatarajiwa kujadili hali mbali mbali ikiwa ni pamoja na uwezekano wa msimu kufutwa kabisa. Lakini Fernando Carro mtendaji mkuu wa Bayer Leverkusen ameliambia shirika la habari la DPA: "kufutwa kwa mashindano yote kwa sababu nyingi sio jambo linalofikiriwa."
Kamati ya kimataifa ya Olimpiki IOC, itafanya mazungumzo na wakuu wa mashirika la kimataifa ya michezo kesho Jumanne katika juhudi za kuchukua hatua dhidi ya kuzuka kwa virusi vya Corona, duru karibu na shirikisho hilo la kimataifa limesema katika taarifa yake.
Ikiwa chini ya miezi mitano hadi kuanza kwa mashindano ya Olimpiki mwaka 2020 mjini Tokyo hapo Julai 24, maswali yamezuka kuhusiana na iwapo michezo hiyo kwamba inaweza kufanyika ama la. Wakati huo huo michuano ya kufuzu kucheza katika michezo hiyo ya olimpiki kwa wana masumbwi kutoka barani Ulaya itafanyika mjini London leo bila mashabiki licha ya wasi wasi unaoongezeka kuhusiana na virusi vya Corona na kuparaganyika kwa kiasi kikubwa kwa matukio ya michezo duaniani kote.
Virusi ambavyo vimeanzia huko nchini China mwishoni mwa mwaka jana, vimewauwa zaidi ya watu 6,000 duniani kote na kuwaambukiza zaidi ya watu 160,000.
Kuzuka kwa virusi hivyo kumeleta mtafaruku katika kalenda ya michezo duniani , na kusababisha kufutwa kwa michuano ya kufuzu kucheza katika michezo hiyo ya Olimpiki na wasi wasi umeongezeka juu ya iwapo michezo yote inapaswa kufutwa ama kuahirishwa.
Hali ya shaka shaka inaongezeka nchini Japan juu ya michezo hiyo ya Olimpiki, kukiwa na upinzani mkubwa wa kutaka kuendelea na michezo hiyo kama ilivyopangwa na wengine wakiwataka maafisa kutohatarisha maisha kwa kulazimisha kuendelea na michezo hiyo katika wakati huu wa dharura ya virusi vya Corona.
Maafisa kama waziri mkuu wa Japan Shinzo Abe na mkuu wa kamati ya kimataifa ya Olimpiki Thomas Bach wamekwisha sisitiza mara kadhaa kwamba matayarisho yaendelee kuwasha mwenge wa olimpiki hapo Julai 24.