Viongozi wa Afrika watoa mpango wa usuluhishi Libya
2 Julai 2011Viongozi wa Afrika wamekubaliana jana Ijumaa kuhusiana na mpango wa amani ambao unamuweka kando ya mazungumzo kiongozi wa Libya, kanali Muammar Gaddafi na waasi. Mpango huo tayari umewasilishwa kwa pande zote kwa matumaini kuwa unaweza kuelekeza katika hatua ya mazungumzo.
Mpango huo unajumuisha Gaddafi kutoa ahadi ambapo atakubali hatua za majadiliano , na kukubali kwake kuwa hatakuwa sehemu ya hatua ya majadiliano, kwa mujibu wa waraka huo. Mpango huo hautoi wito kwa Gaddafi kujiuzulu, ambalo ni dai kuu la waasi katika baraza la taifa la mpito ambalo limesisitiza katika mkutano huo kuwa Gaddafi ni lazima aondoke kwa vyovyote vile, hata kama utapatikana muafaka wa kisiasa katika mzozo huo uliodumu miezi minne sasa.
Mkutano huo wa kilele pia umeamua kutotekeleza waranti uliotolewa na mahakama ya kimataifa ya uhalifu dhidi ya Gaddafi, mtoto wake na mkuu wa idara ya upelelezi , ambao wamesema unatatiza juhudi za kuleta suluhisho.
Tumepata fursa muda mfupi uliopita kukabidhi rasmi kwa ujumbe wa pande zote mapendekezo yetu ili wayapeleke kwa wenzao, rais wa Afrika kusini Jacob Zuma amewaambia waandishi habari. Ameongeza kuwa wamepokea mapendekezo hayo kwa moyo mkunjufu. Tuna furaha kuwa tumefikia katika hatua hii, ambayo tunaweza sasa kusema hivi karibuni tutaanzisha mazungumzo mjini Addis Ababa na tunaamini tutapata uungwaji mkono kutoka kwa kila mmoja, amesema rais Zuma.
Mpango huo unatoa wito wa kusitishwa mara moja mapigano, usitishaji wa hali ya kiutu, usitishaji kamili, maridhiano ya kitaifa, mipango itakayohusiana na hatua za mpito, pamoja na angenda kwa ajili ya mabadiliko ya kidemokrasia. Miji yote ni lazima iachwe huru bila kuzingirwa na majeshi, mashambulio yasitishwe na watu ambao wamekamatwa wakati wa mzozo huo waachiwe huru, umeeleza waraka wa mpango huo.
Pia waraka huo umeeleza kuwa umoja wa mataifa unapaswa kuondoa marufuku ya kuruka ndege za Libya katika anga lake, hatua ambayo imesababisha mashambulio yaliyoongozwa na NATO dhidi ya majeshi ya Gaddafi, na umoja wa Afrika pamoja na jumuiya ya mataifa ya Kiarabu , zitatuma vikosi vya kutosha vya jeshi la kulinda amani.
Mpango huo pia unaeleza kuwa kipindi cha mpito kitajumuisha siku 30 za majadiliano ya kitaifa, ambayo yataelekeza katika uchaguzi na pia kuruhusu msamaha .
Jumuiya ya kimataifa itachunguza juu ya kutimizwa kwa usitishaji wa mapigano, kuondoa vikwazo na kuondoa hatua ya kuzuwia mali za Libya nchi za nje. Lakini ujumbe wa waasi umesisitiza siku ya Alhamis kuwa ili mazungumzo yoyote yaanze, Gaddafi ni lazima aondoke, dai ambalo maafisa wa umoja wa Afrika wamesema linaweza kuletwa katika meza ya majadiliano. Mwakilishi wa baraza la taifa la mpito Mansour Safy al-Nasr amesema kuwa waasi wataendelea kupigana hadi pale Gaddafi atakapoondoka, lakini pia watasitisha mapigano iwapo ataondoka.
Iwapo tutaona kuwa Gaddafi anajiondoa , tuko tayari kuacha mapigano na kujadiliana na ndugu zetu ambao wako karibu ya Gaddafi, amesema Nasr.
Kiongozi wa ngazi ya juu wa waasi nchini Libya Mahmud Jibril amewataka viongozi wa umoja wa Afrika kuchukua msimamo uliowazi dhidi ya Gaddafi baada ya mahakama ya kimataifa ya uhalifu kutoa waranti wa kukamatwa Gaddafi siku ya Jumatatu. Lakini mkutano huo umeamua kuwa mataifa ya Afrika hayatatekeleza waranti huo , umeeleza waraka wa ufupisho wa maamuzi hayo.
Mwandishi : Sekione Kitojo / afpe
Mhariri : Thelma Mwadzaya