1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa AU waupa nguvu umoja huo

Kabogo Grace Patricia3 Julai 2009

Viongozi wakuu wa AU, wameidhinisha mpango wa kuimarisha zaidi mamlaka ya umoja huo na kuratibu sera za ulinzi na biashara

https://p.dw.com/p/IgQa
Kiongozi wa Libya, Muammar Ghaddafi, ambaye ndiye mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU), akiwa mbele ya bendera za nchi wanachama wa AU.Picha: AP

Mwenyekiti wa mkutano huo, Muammar Ghaddafi, kiongozi wa Libya, amekuwa akiutaka umoja huo kuwa jumuia moja kama ulivyo Umoja wa Ulaya na kushinikiza kupitishwa kwa mipango kadhaa iliyokuwa katika ajenda kuu za mkutano huo.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Benin, Jean-Marie Ehouzou, amewaambia waandishi habari kuwa waraka huo unaoipa bodi ya umoja huo mamlaka zaidi umepitishwa baada ya majadiliano ya muda mrefu. Amesema kwa pamoja wamekubaliana kuratibu masuala ya kigeni na ulinzi.

Amesema waraka huo ulitakiwa kuridhiwa na mabunge ya nchi wanachama kabla ya kuidhinishwa. Amebainisha kuwa mataifa ya Afrika yako tayari kutoa japo kidogo rasilimali zake kwa ajili ya faida ya umoja huo.

Kwa mujibu wa waraka huo, Umoja wa Afrika (AU) utaratibu nafasi za nchi wanachama wakati wa majadiliano ya kimataifa, kutekeleza sera ya pamoja ya Afrika ya ulinzi na usalama pamoja na kuhamasisha uwepo wa mikakati ya maliasili muhimu kwa ulinzi wa bara la Afrika.

Umoja huo ulioanzishwa mwaka 1999 katika mji wa Sirte, Libya, ukiwa na wanachama 53, ulikuwa na lengo la kupiga vita umasikini na udhaifu kwa kuondoa vikwazo vya kibiashara na kuruhusu mataifa ya Afrika kuzungumza lugha moja.

Umoja huo pia unajadili maazimio ya kisiasa na kuangalia vikosi vyake vya kulinda amani vilivyopo nchini Somalia na katika jimbo la Darfur, Sudan.

Hadi sasa umoja huo unakabiliwa na matatizo kadhaa yakiwemo ushuru wa forodha, vizuizi vya mipaka na miundombinu mibovu ya usafiri inayosababisha mataifa ya Afrika kutosonga mbele katika sekta ya biashara.

Mataifa mengi ya Afrika yanaunga mkono kuwa na uchumi wa aina moja, lakini baadhi ya mataifa yana wasiwasi juu ya jukumu la kisiasa iliyopewa Umoja wa Afrika, kwa sababu hakuna nchi yoyote iliyo tayari kupoteza madaraka katika sera za kigeni na ulinzi.

Mwanadiplomasia mmoja anayehudhuria mkutano huo unaomalizika hii leo, amesema anautilia shaka waraka huo kutokana na kutotambua hasa mamlaka mapya ya umoja huo.

Kwa mujibu wa mwanadiplomasia huyo, bodi hiyo ya Umoja wa Afrika itaratibu masuala muhimu ya umoja huo, lakini haitakuwa na mamlaka ya kufanya maamuzi bila kuzishirikisha nchi wanachama.

Mwezi Februari mwaka huu, viongozi wa nchi 53 za Umoja wa Afrika walikubaliana kuunda mamlaka ya AU, kutoka Kamisheni ya AU, lakini Ghaddafi alishinikiza iundwe bodi itakayotazama namna ya kuunganisha ulinzi, biashara na uhusiano wa kigeni.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (RTRE/AFPE)

Mhariri: Abdul-Rahman