1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa dini ya kiislamu na kiyahudi wakutana Italia

Amina Abubakar Daniel Gakuba
16 Septemba 2019

Maimamu wa Kiislamu na viongozi wa dini ya kiyahudi kutoka barani Ulaya wanahudhuria mkutano wa kilele nchini Italia ulioandaliwa na baraza la waislamu na wayahudi kujadili masuala yanayowaathiri. 

https://p.dw.com/p/3Pf5R
Meet2resepct-Demo in Berlin: Juden und Muslime radeln gemeinsam
Picha: AFP/Getty Images/J. MacDougall

Kuanzia jana Jumapili viongozi wa kiyahudi na wale wa dini ya kiislamu kutoka mataifa 15 wamekutana mjini Matera Kusini mwa Italia, moja ya miji ya kitamaduni ya ulaya mwaka huu wa 2019 kuwa mwenyeji wa mkutano huo wa kilele wa viongozi hao wa kidini. Viongozi hao wanaweka msingi itakaowawezesha kuzungumzia kwa pamoja na kwa uwazi zaidi maswala yanayowaathiri.

"Nadhani mpango huu ni mpangilio wa kipekee unaopaswa kukuzwa na kuungwa mkono," alisema Tarafa Baghajati, Mhandisi kutoka Vienna na mmoja wa Maimamu mashuhuri nchini Austria.

Mambo muhimu yatakayojadiliwa katika mkutano huo ni pamoja na chuki dhidi ya wayahudi, Ubaguzi dhidi ya uislamu na ongezeko la siasa kali za mrengo wa kulia.

Mkutano huu wa sasa unaofanyika mjini Matera unawasilisha muelekeo mpya katika majadiliano ambayo kwa kawaida yanagubikwa na mgogoro wa Mashariki ya Kati. Maimamu wa dini ya kiislamu na viongozi wa dini ya kiyahudi kutoka  Ireland hadi Ugiriki, Romania, Lithuania na Portugal wanahudhuria.

Katibu mkuu wa mkutano wa viongozi wa kiyahudi wa Ulaya Gady Gronich ameiambia DW kwamba kwa kuchagua mji wa Matera, viongozi hao walitaka kutoa ujumbe mzito kuwa wote ni sehemu ya utamaduni wa Ulaya.

Viongozi hao wanawasiwasi juu ya kushamiri kwa vyama vya siasa kali za mrengo wa kulia

Faraway so close
Picha: AP

Gronich ameongeza kuwa Italia kama mataifa mengine barani Ulaya inayotawaliwa na serikali ya siasa kali za mrengo wa kulia, hivi karibuni iliazimia kudhibiti taratibu za kidini zinazohusiana na kuchinjwa wanyama  na kutahiriwa vijana wadogo, ambayo mambo yote mawili yanafanyika katika dini ya uislamu na ile ya kiyahudi. Amesema kwa sasa azma hiyo ya serikali imewekwa kando.

Jamii zote mbili za wasilamu na wayahudi zinawasiwasi kuhusu njia za kisiasa zinazotumika kuingilia masuala ya kiimani. Gronich amesema wanania ya kuanzisha kamati mpya itakayokuwa na wawakilishi wawili kutoka kila upande wa kidini akimaanisha upande wa kiislamu na upande wa kiyahudi, kamati itakayokuwa na jukumu la kujadili masuala tete pamoja na wanasiasa wa Umoja wa Ulaya.

Tarafa Baghajati, Imamu kutoka Austria pia amezungumzia majaribio ya kudhibiti shughuli za kidini na mara moja akagusia umaarufu wa vyama vya siasa kali barani Ulaya.

Amegusia chama kinachopinga uhamiaji cha cha Alternative for Deutschland, AfD vyama vya mrengo wa kulia vya Austria, chama cha Ligi cha Matteo Salvini nchini Italia na chama cha PVV nchini Uholanzi, akisema makundi kama haya yanaongeza chuki na ubaguzi dhidi ya uislamu hasa dhidi ya wahamiaji.

Chanzo: DW