1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa dunia kuadhimisha miaka 75 ya D-Day

Daniel Gakuba
5 Juni 2019

Rais Donald Trump ataungana leo na viongozi wa nchi 16 katika kuadhimisha miaka 75 tangu kuanza kwa operesheni ya kijeshi iliyoikomboa Ulaya kutoka mikononi mwa Wanazi wa Ujerumani, maarufu kama D-Day.

https://p.dw.com/p/3Jru7
Großbritannien D-Day-Gedenkveranstaltung in Portsmouth
Picha: Reuters/C. Barria

Trump atakuwa pamoja na wenyeji wake, Malkia Elizabeth II na Waziri Mkuu Theresa May, na pia Kansela wa Ujerumani Angela Merkel katika maadhimisho hayo yanafanyika katika mji wa Portsmouth Kusini mwa Uingereza.  Wakongwe 300 walioshiriki katika operesheni hiyo watahudhuria pia. 

Tarehe kama ya leo mwaka 1944, wanajeshi 170,000 wa nchi washirika walivuka bahari na kutua kwenye fukwe za Normandy nchini Ufaransa, ikawa mwanzo wa mwisho wa utawala wa Wanazi wa Ujerumani waliokuwa wameyakalia maeneo makubwa ya Ulaya katika vita vikuu vya pili.

Heshima kwa mashujaa

Großbritannien D-Day-Gedenkveranstaltung in Portsmouth
Wazee 300 walioshiriki katika operesheni ya D-Day wameshiriki maadhimisho hayoPicha: picture-alliance/dpa/K. Nietfeld

Rais Donald Trump anatarajiwa kutoa heshima kwa wanajeshi waliouawa katika vita hivyo, kabla ya kuondoka Uingereza akielekea Ireland. Katika mkutano na waandishi wa habari jana mjini London, Trump alisema anayo heshima kubwa kwa wanajeshi hao, aliowataja kama 'mashujaa waliojitolea maisha yao kuunusuru ustaarabu'. Alisema urafiki uliotengenezwa wakati wa operesheni hiyo, na kuimarishwa na damu iliyomwagika, utadumu milele.

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel, Waziri Mkuu wa Canada Justin Trudeau na Rais wa Ufaransa ni miongoni mwa viongozi wengine watakaoshiriki katika maadhimisho hayo yanayoongozwa na Waziri Mkuu Theresa May na Malkia Elisabeth II.

Mwanzo wa mwisho wa utawala wa Wanazi

D-Day Archivbilder Juno Beach
Wanajeshi wapatao 170,000 walihusishwa katika operesheni hii.Picha: Reuters/National Archives of Canada/Ken Bell

Mashambulizi yaliyoanza siku ya D-Day dhidi ya wanajeshi wa Ujerumani waliokuwa wakiikalia kimabavu Ufaransa, ndio operesheni kubwa zaidi ya kutokea baharini katika historia ya dunia. Yalitokea wakati sehemu kubwa ya wanajeshi wa Ujerumani ikipambana na Umoja wa Kisovieti sehemu ya Mashariki, na operesheni hii kutokea Magharibi  iligeuza mkondo wa vita ulioendelea hadi kuangushwa kwa Adolf Hitler na utawala wake wa kinazi.

Sambamba na maadhimisho hayo, wanajeshi wa Uingereza watafanya luteka za kijeshi mjini Portsmouth, zitakazohusisha manowari 11 na ndege 26 za kijeshi.

Kabla ya maadhimisho hayo, nchi 16 zinazoshiriki zimewekeana ahadi mpya ya kufanya kazi pamoja kama marafiki na washirika. Tangazo la pamoja la nchi hizo limesema nchi hizo zimeshirikiana katika muda wa miaka 75 iliyopita kusimamia amani barani Ulaya na kote ulimwenguni, na kuwa wadhamini wa demokrasia, utawala wa sheria na kuvumiliana. Hali kadhalika wametoa shukrani wa wapiganaji walioshiriki katika operesheni ya D-Day ambao bado wako hai, na kutoa heshima kwa waliofariki.

 

AP, AFP, dpa