Viongozi wa ECOWAS kukutana leo Nigeria kujadili mzozo wa Cote d'Ivoire
7 Desemba 2010Mkutano huo unafanyika wakati kukihofiwa kutokea ghasia na tishio la nchi hiyo kuwekewa vikwazo, huku wapatanishi wa kimataifa wakitafuta suluhu kumaliza mzozo huo.
Hata hivyo viongozi wa Cote d'Ivoire hawakualikwa katika mkutano huo wa wanachama 15 wa Jumuiya ya Kiuchumi ya nchi za Afrika magharibi -ECOWAS- unaofanyika nchini Nigeria, licha ya kwamba nchi hiyo ni mwanachama wa jumuiya hiyo.
Tayari Jumuiya hiyo ya -ECOWAS- imetoa taarifa kuhusiana na mzozo huo, ikimlaumu Rais anayemaliza muda wake Laurent Gbagbo na kutoa wito wa kukubali matokeo ya uchaguzi yanayoonesha kuwa mpinzani wake Alassane Ouattara alishinda katika uchaguzi wa rais.
Wakati mkutano huo wa viongozi wa nchi za Afrika magharibi ukifanyika leo, Rais wa zamani wa Afrika kusini Thabo Mbeki, jana alishindwa kumaliza mvutano uliopo kati ya Alassane Ouattara anayedai kuwa ndiye rais mpya wa Cote d'Ivoire, na rais Laurent Gbagbo. Hata hivyo, amewataka viongozi hao kutafuta suluhisho la amani.
Wakati Jumuiya ya Kimataifa ikichukua jitihada kuumaliza mzozo huo wa Cote d'Ivoire, Mwendesha mashtaka mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa kivita, Luis Moreno Ocampo, ameitaka nchi hiyo kuchukua hatua kumaliza mzozo huo na kuzuia uwezekano wa kutokea uhalifu wa kivita au uhalifu dhidi ya ubinadamu, kufuatia uchaguzi wa urais uliozusha mzozo.
Kwa upande wake Rais wa Marekani Barack Obama, amemtaka rais anayemaliza muda wake Laurent Gbagbo kukabidhi madaraka, kwa mshindi halali wa uchaguzi huo.
Afisa wa ngazi ya juu wa Marekani, amesema Ikulu ya nchi hiyo inamtambua Bwana Ouattara kama mshindi halali wa uchaguzi wa Rais wa Cote d'Ivoire.
Takriban watu 20 wamekufa katika ghasia zinazohusiana na uchaguzi nchini humo huku kukiwa na hali ya wasiwasi, kutokana na mkwamo kati ya mahasimu wawili wakubwa rais Gbagbo na mpinzani wake, Allasane Ouattara, ambaye ni waziri mkuu wa zamani.
Rais anayemaliza muda wake Laurent Gbagbo ameikataa miito ya kimataifa, kumtaka kumaliza mudwa wake wa miaka 10 madarakani, baada ya Umoja wa Mataifa kumtambua Alassane Ouattara kama mshindi wa uchaguzi huo wa Rais, ambao ulitakiwa kuleta amani nchini humo, lakini badala yake kuibua machafuko ya umwagaji damu.
Wakati huo huo, Msemaji wa Umoja wa Mataifa Martin Nesirky amesema umoja huo unawahamisha baadhi ya wafanyakazi walioko nchini Cote d'Ivoire kutokana na sababu za kiusalama. Baadhi ya wafanyakazi 460 wa umoja huo watapelekwa kwa muda nchini Gambia, ambako wataweza kuendelea na kazi yao.
Mwandishi: Halima Nyanza(dpa, afp,ap, reuters)
Mhariri: Josephat Charo