Viongozi wa EU wakubaliana ushirikiano wa wazi na Uingereza
15 Oktoba 2020Ni kwa mara ya tatu tangu kutokea kwa mlipuko wa janga la virusi vya corona ambapo viongozi wa Umoja wa Ulaya wanakutana ana kwa ana mjini Brussels. Huku wakivaa barakoa na walitengana kwa kuweka umbali baina yao wakati walipokutana ili kujadili hatua ya Brexit, kuhusu mkataba wa kibiashara.
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amesema wanataka makubaliano lakini siyo kwa gharama yoyote na wanaomba kuweko kwa mkataba ulio sawa unaozingatia maslahi ya pande mbili.
Kwa upande wake rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amesema kwamba mkataba na Uingereza ni muhimu kwa pande zote mbili.
Uingereza ilijiondoa kwenye Umoja wa Ulaya mwezi Januari na washirika hao wawili wa zamani wamekuwa kwenye mazungumzo magumu kujaribu kuendesha biashara bila haki za forodha na mafungu ifikapo mwaka 2021.
Mazungumzo yalisababisha kuweko na maelewano kuhusu masuala ya ustawi wa jamii na usafiri, lakini suala la ushindani halali, ufumbuzi wa tofauti na uvuvi ambao ni muhimu hasa kwa Ufaransa, vinaendelea kuzigawa pande mbili hizo.
Kuhusu janga la virusi vya corona, Umoja wa Ulaya unataka kuweko na kanuni za pamoja kuhusu vizuwizi na vipimo kwenye nchi wanachama wa umoja huo. Rais wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya, Ursula Von der Leyen amesema leo kwamba hali ya maambukizi ya corona inatisha barani Ulaya.
Hofu imeongezeka Alhamis kuwa Ulaya inapoteza fursa za kuudhibiti mripuko wa virusi vya corona katika kipindi hiki cha vuli, wakati maambukizi yanayorekodiwa kwa siku yakifika kiwango cha juu zaidi nchini Ujerumani, Jamhuri ya Czech, Ubelgiji, Uhispania, Uholanzi, Italia na Poland. Ufaransa imetangaza amri ya kutotembea nje kuanzia saa tatu usiku katika miji yake mikubwa. Nao wakaazi wa London wakikabiliwa na vizuizi vipya vya kusafiri wakati serikali zikiweka kanuni mpya kali.