1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa G20 wakosa kuafikiana kuihusu Syria

6 Septemba 2013

Viongozi wa nchi zenye nguvu zaidi kiuchumi duniani wameshindwa kuafikiana kuhusu mzozo wa Syria katika mkutano unaofanyika nchini Urusi huku Marekani ikitafuta uungwaji mkono kuchukua hatua za kijeshi dhidi ya Syria

https://p.dw.com/p/19css
Picha: Reuters

Katika dhifa ya chakula cha jioni hapo jana mwenyeji wa mkutano huo Rais wa Urusi, Vladimr Putin, aliwaalika viongozi wenzake kulijadili suala la Syria ambalo linaonekana kufunika ajenda rasmi za mkutano huo ambayo ni masuala ya kiuchumi na biashara.

Viongozi walipata fursa ya kulizungumzia suala hilo la Syria kwa saa tatu huku kila mmoja akitengewa dakika kumi kueleza msimamo wake kulihusu. Waziri mkuu wa Italia, Enricco Letta, alithibitisha kupitia mtandao wa twitter kuwa hakukuwa na maafikiano kuhusu mzozo wa Syria.

Urusi imekuwa ikisimama kidete kuhusu kutochukuliwa hatua za kijeshi dhidi ya utawala wa Rais Bashar al Assad kuhusiana na madai kuwa ulitumia silaha za kemikali dhidi ya raia wake tarehe 21 mwezi uliopita.

Urusi yasimama kidete

Mjumbe wa Marekani kwa umoja wa Mataifa, Samantha Power, ameishutumu Urusi kwa kulishika mateka baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kwa kutumia kura yake ya turufu. Waziri mkuu wa Uingereza, David Cameron, naye amesema nchi yake ina ushahidi mpya kuhusu shambulio hilo la kemikali.

Rais wa Urusi Vladimir Putin(Kushoto)na katibu mkuu wa umoja wa Mataifa Ban ki Moon
Rais wa Urusi Vladimir Putin(Kushoto)na katibu mkuu wa umoja wa Mataifa Ban ki MoonPicha: Getty Images

Katibu mkuu wa umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, amewaambia viongozi hao wa G20 kuwa kutoa silaha kwa upande wowote katika mzozo wa Syria sio suluhisho kwani hatua za kijeshi haziwezi kuwa suluhisho la mzozo huo.

Kikao hicho wakati wa chakula cha jioni hakikutarajiwa hata hivyo kuibuka na maazimio yoyote kuhusu mzozo wa Syria. Duru zinaarifu kuwa waliohudhuria walilaani matumizi ya silaha za kemikali lakini pia walitaka kujua hasa ni upande gani katika mzozo huo ulizitumia.

Washirika wa Syria hawaonekani kushawishika na kampeini za Obama za kuchukuliwa hatua za kijeshi. Obama hii leo anatarajiwa kukutana na Rais wa China pembezoni mwa mkutano huo kulijadili suala la Syria miongoni mwa masuala mengine na baadaye kukutana na mshirika wake Rais wa Ufaransa, Francois Hollande.

Syria yafunika ajenda ya G20

Naye Cameron amekutana na Putin kulijadili suala hilo la Syria. China imekuwa ikitumia kura yake ya turufu katika baraza la usalama kupinga hatua kuchukuliwa dhidi ya Syria.

Rais wa Urusi Vladimir Putin akimkaribisha Rais wa Marekani Barrack Obama katika mkutano wa G20
Rais wa Urusi Vladimir Putin akimkaribisha Rais wa Marekani Barrack Obama katika mkutano wa G20Picha: picture-alliance/dpa

Kiongozi mkuu wa kidini wa Iran, Ayatollah Khamenei, ameyataja madai ya kutumika silaha za kemikali mjini Damscus kama kisingizio cha kuishambulia Syria na kuahidi kuiunga mkono nchi hiyo hadi mwisho.

Kiongozi wa kanisa Katoliki duniani, Baba mtakatifu Francis, pia ameelezea hisia zake kuhusu mzozo huo na kutoa wito kutafutwe suluhisho la amani na wala si kwa kutumia nguvu za kijeshi akionya hatua za kijeshi zitaambulia patupu katika kuumaliza mzozo wa Syria.

Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel, amesema mara kadhaa kuwa nchi yake haitashiriki katika shambulio la kijeshi litalaoongozwa na Marekani dhidi ya Syria na tayari bunge la Uingereza lilipiga kura kupinga nchi hiyo pia kuhusika katika hatua hiyo.

Mwandishi:Caro Robi/afp/ap

Mhariri: Josephat Charo