Viongozi wa G20 waelekea India kwa mkutano wa kilele
8 Septemba 2023Viongozi waliogawika wa kundi la nchi tajiri na zile zinazoinukia kiuchumi la G20, wanaelekea mjini New Delhi India leo kwenye mkutano wa kilele ambapo Rais wa China Xi Jinping na Rais wa Urusi Vladimir Putin wanasemekana kuwa hawatoshiriki. Ikulu ya Urusi Kremlin imearifu pia kwamba Rais Putin hana mpango hata wa kuhutubia kwa njia ya video katika mkutano huo wa siku mbili.
Rais wa Marekani Joe Biden anatumai kutumia nafasi ya kukosekana kwa viongozi wa China na Urusi ili kuimarisha ushawishi wa Washington.
Viongozi hao wanakutana wakati kukiwa na mgawanyiko mkubwa haswa kuhusu vita vya Ukraine na jinsi ya kuyasaidia mataifa yanayoinukia kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi. Waziri Mkuu wa India Narendra Modi amesisitiza dhamira ya kutanua kundi hilo kwa kujumuisha Umoja wa Afrika kama mwanachama wa kudumu.