Viongozi wa G7 wakamilisha mkopo wa Ukraine
26 Oktoba 2024Wakuu wa mataifa ya G7 wamesema wamefikia makubaliano juu ya namna ya kuufikisha mkopo huo, wakilenga kuanza kuupeleka kupitia chaneli mbalimbali, mwishoni mwa mwaka huu.
Wamesema utatumika kwa ajili ya kusaidia bajeti ya Ukraine, jeshi na msaada wa kujijenga upya.
Wanatoa tangazo hilo wakati mawaziri wa fedha wakiwa wamekusanyika mjini Washington wiki hii kwa ajili ya mikutano iliyoandaliwa na Shirika la Kimataifa la Fedha, IMF na Benki ya Dunia.
Wakuu hao walikubaliana katika mkutano wa mwaka wa kilele uliofanyika kusini mwa Italia mnamo mwezi Juni, kuipatia Ukraine mikopo itakayotokana na faida ya mali za Urusi zilizozuiwa, lakini baadhi ya masuala ya kiufundi yalikuwa bado hayajawekwa sawa.
Mali za Urusi za kiasi cha dola bilioni 280.62 kama akiba ya Benki Kuu zilizuiwa chini ya vikwazo ilivyowekewa taifa hilo, kufuatia uvamizi wa Moscow nchini Ukraine mnamo Februari 2022.