Viongozi wa mapinduzi Guinea wawaachia wafungwa wa kisiasa
8 Septemba 2021Hayo yanafanyika wakati ambapo Jumuiya ya Uchumi ya nchi za Afrika Magharibi, ECOWAS ikijiandaa siku ya Jumatano kuujadili mzozo wa taifa hilo.
Kikosi hicho kinachoongozwa na Kanali Mamady Doumbouya kilifanya mapinduzi siku ya Jumapili na kumkamata Rais Conde, hatua iliyosababisha ukosoaji mkubwa wa kimataifa, ikiwemo Marekani, Umoja wa Ulaya na ECOWAS.
Mwandishi habari wa shirika la habari la Ufaransa, AFP amesema aliwaona takribani wafungwa 20 wakiachiwa huru kutoka gerezani kwenye mji mkuu wa Guinea, Conakry jana jioni, wakiwemo wanaharakati maarufu wa upinzani.
Mawakili wanaowatetea wafungwa hao wamesema watu 79 wamekamilisha taratibu za kuachiliwa huru baada ya kufanya mazungumzo na jeshi. Ismael Conde, mwanaharakati wa chama cha upinzani cha UFDG ambaye ni miongoni mwa wapinzani walioachiwa huru, amesema wanamuomba Mungu kwamba huo uwe mwanzo mpya kwa Guinea.
"Halikuwa jambo jepesi, miezi 12 sio siku 12 au wiki 12, tunazungumzia miezi 12 ya kuwa gerezani, ya ukosefu wa haki. Ni hisia ambayo huwezi kuielezea, tumerudi kuungana na familia zetu leo," alifafanua Conde.
Guinea yenye demokrasia
Mwanaharakati huyo wa upinzani amesema anaomba kusiwe na raia mwingine wa Guinea ambaye atafungwa gerezani kwa sababu kama zao. Conde amesema wameachiwa huru wakiwa na nguvu za kuendeleza mapambano kwa ajili ya Guinea huru na yenye demokrasia.
Siku ya Jumatatu, jeshi lilitoa taarifa ikiitaka wizara ya sheria kuharakisha mchakato wa kuachiwa huru wafungwa wa kisiasa. Siku ya Jumanne, Kanali Doumbouya pia alirejea ahadi yake ya kufanya mazungumzo ya kuunda serikali mpya.
Kiongozi huyo wa mapinduzi aliandika katika ukurasa wake wa mtandao wa Twitter kwamba serikali itakayoundwa, itakuwa ya umoja wa kitaifa na itahakikisha kunakuwepo na kipindi cha mpito cha kisiasa.
Hata hivyo, hadi sasa bado haijajulikana mahali aliko Alpha Conde, ingawa viongozi wa mapinduzi wamehakikisha kuwa yuko salama.
Kiongozi wa chama kikuu cha upinzani nchini Guinea, Cellou Dalein Diallo ameunga mkono mapinduzi hayo kwa matumaini kwamba yatasaidia kupatikana kwa demokrasia ya amani kwenye taifa hilo lenye watu milioni 13.
Siku ya Jumatatu, muungano wa upinzani wa Diallo wa ANAD ulilitolea wito jeshi linalotawala kuanzisha taasisi halali zenye uwezo wa kuleta mageuzi na kuheshimu utawala wa sheria.
Baada ya kuchukua madaraka, viongozi wa mapinduzi waliivunja katiba ya Guinea pamoja na serikali. Siku ya Jumanne wanajeshi walianza kuondoa vizuizi vya polisi na jeshi kwenye mji mkuu, ambavyo wakosoaji wa Conde wamesema viliwekwa ili kudhibiti maandamano.
Ama kwa upande mwingine, Urusi imezitaka taasisi zote za Guinea ziruhusiwe kufanya kazi haraka iwezekanavyo. Msemaji wa Ikulu ya Urusi, amesema wanatarajia kwa hali yoyote ile kwamba maslahi ya wafanyabiashara wao hayatoathiriwa.
(AFP, Reuters)