Viongozi wa SADC wakutana katika mkutano wa dharura
27 Mei 2021Viongozi wa jumuiya ya maendeleo ya kiuchumi ya nchi za Kusini mwa Afrika-SADC watafanya kikao maalum cha mkutano wa kilele hii leo mjini Maputo nchini Msumbiji kujadili machafuko yanayolikumba eneo la kaskazini mwa nchi hiyo.Kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa na Ofisi ya rais wa Afrika Kusini jana ni kwamba rais Cyril Ramaphosa ataongoza ujumbe wa nchi yake katika mazungumzo hayo.
Mkutano huo wa mafisa wa ngazi za juu uliakhirishwa mnamo mwezi Aprili kutokana na migogoro iliyokuwepo. Mkutano huo wa leo utajadili hali ya ugaidi inayolikumba eneo hilo ikiwemo ukosefu wa usalama katika mkoa wa Cabo Delgado katika jamhuri ya Msumbiji. Aidha kikao hicho kinatarajiwa kujadili uwezekano wa jumuiya hiyo ya SADC kupeleka wanajeshi 3,000 kwenda kukabiliana na uasi. Machafuko yanayosababishwa na makundi ya itikadi kali yamezagaa katika eneo hilo la kaskazini mwa msumbiji lenye utajiri wa gesi tangu yalipozuka kwa mara ya kwanza mwishoni mwa mwaka 2017.