Umoja wa Ulaya umeidhinisha makubaliano ya Brexit
25 Novemba 2018Viongozi wa Umoja wa Ulaya waliokutana mjini Brussels, Ubelgiji wameidhinisha makubaliano ya Uingereza kujitoa katika umoja huo ifikapo mwakani. Hii ni mara ya kwanza kwa nchi kujitoa katika muungano huo wenye nchi wanachama 28 kwa sasa. Katika mkutano huo wa kilele, Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May amesema makubaliano hayo ni mwanzo mpya kwa Uingereza, lakini Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya.
Jean-Claude Juncker amesema kuondoka kwa Uingereza ni janga. Msimamizi mkuu wa makubaliano hayo kwa Umoja wa Ulaya Michel Barnier amesema awamu ya kwanza ya makubaliano imekamilika, Uingereza na Umoja wa Ulaya zinahitaji kufanya kazi pamoja ili kujenga ushirikiano mpya. Makubaliano hayo yanahitaji kuidhinishwa na bunge la Uingereza. Idadi kubwa ya wabunge wa pande zote mbili - wanaopinga na wanaounga mkono Uingereza kujitoa katika Umoja wa Ulaya- wanatishia kuyapinga makubaliano hayo yatakapowasilishwa bungeni mwezi ujao.