1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa Umoja wa Ulaya waidhinisha makubaliano ya Brexit

Oumilkheir Hamidou
25 Novemba 2018

Viongozi wa Umoja wa Ulaya wameunga mkono makubaliano ya kujitenga Uingereza na Umoja huo pamoja pia na mkataba wa uhusiano wa siku za mbele kati ya pande hizo mbili.

https://p.dw.com/p/38sJK
EU-Sondergipfel zum Brexit in Brüssel
Picha: Reuters/Y. Herman

"Viongozi wa mataifa 27 yaliyosalia ya Umoja wa Ulaya wameunga mkono makubaliano na azimio la kisiasa kuhusu uhusiano wa siku za mbele kati ya Umoja wa Ulaya na Uingereza", ameandika mwenyekiti wa baraza la Ulaya Donanld Tusk katika mtandao wake wa kijamii wa Tittwer, akigusia nyaraka mbili zilizotiwa saini leo mjini Brussels.

Majadiliano yaliendelea hadi dakika ya mwisho kuhusu nyaraka hizo zinazohalalisha kujitoa rasmi Uingereza kutoka Umoja wa Ulaya Machi 19 mwaka 2019, pamoja pia na kufungua njia ya kuanza mazungumzo kuhusu mustakbali wa uhusiano wa siku za mbele tangu wa kisiasa mpaka wa kibiashara.

 

Viongozi wa Umoja wa Ulaya wakijadiliana kuhusu Brexit mjini Brussels
Viongozi wa Umoja wa Ulaya wakijadiliana kuhusu Brexit mjini BrusselsPicha: Reuters/O. Hoslet

 Brexit ni majonzi makubwa,anasema Jean-Claude Juncker

 

Waziri mkuu Theresa May anakabiliwa na mtihani mkubwa sasa wa kuwatanabahisha wabunge wa Uingerezua waunge mkono makubaliano yaliyofikiwa.

Mkataba wa Brexit umezusha lawama kali kutoka kwa wale wanaoupinga Umoja wa Ulaya sawa na wenzao wanaouunga mkono nchini Uingereza ambako yadhihirika kana kwamba hautaungwa mkono utakapofikishwa bungeni kupigiwa kura katikati ya mwezi unaokuja wa Desemba.

Viongozi wa Umoja wa Ulaya wamewatolea wito wabunge wa Uingereza Jumapili waunge mkono makubaliano yaliyofikiwa.

"Kujitoa Uingereza katika Umoja wa Ulaya ni tukio la majonzi makubwa," amesema mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Jean-Claude Juncker. Hata hivyo ameelezea matumaini yake kuona bunge la Uingereza likiunga mkono mkataba huo wa Brexit.

Akiulizwa ushauri wake kwa wabunge wa Uingereza Juncker amesema "angepiga kura kuunga mkono kwasabubu anasema "huo ni mkataba bora zaidi kwa Uingereza".

Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa
Rais Emmanuel Macron wa UfaransaPicha: Imago/Belga/E. Lalmand

Macron ahimiza mageuzi ya kina yafanyike

Umoja wa Ulaya hautabadilisha msimamo wake kuelekea Brexit amesema kwa upande wake kiongozi wa tume ya Umoja wa Ulaya katika mazungumzo ya Brexit, Michel Barnier. Ameyataka makubaliano hayo kuwa hatua inayohitajika katika kubuni hali ya kuaminiana kati ya Uingereza na Umoja wa Ulaya ili kuweza baadae kujadiliana kuhusu uhusiano wa siku za mbele.

Waziri mkuu wa Uholanzi Mark Rutte pia amewatolea wito wabunge wa Uingereza waunge mkono makubaliano hayo. Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa amesema kwa upande wake makubaliano ya Brexit yanabainisha udhaifu wa Umoja wa Ulaya . Amewatolea wito viongozi waunge mkono mageuzi ya kina.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AP

Mhariri: Yusra Buwayhid