Viongozi wakutana kujadili hali ya kibinaadamu
23 Mei 2016Mkutano huo wa kilele unakuja katika wakati ambapo kuna mzozo mkubwa wa wakimbizi duniani na mahitaji ya kibinadamu yakizidi kuongezeka kutokana na mizozo, majanga na mabadiliko ya hali ya hewa. .
Viongozi wa nchi takriban 50, wanasiasa, wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa, wawakilishi wa mashirika yasiyokuwa ya serikali, kampuni binafsi, wafanyakazi wa mashirika ya kutoa misaada na watafiti wanakutana pamoja kwa mkutano huo ulioandaliwa na Umoja wa Mataifa.
Wengi wana matumaini kuwa mkutano huo wa kilele utasaidia katika kuimarisha na kubadilisha sekta ya misaada ya kibinadamu.
Lakini pia kumekuwa na shutuma kuhusu kuandaliwa kwa mkutano huo. Shirika la madaktari wasio na mipaka MSF halihudhurii mkutano huo baada ya kuuita mkutano wa kuficha ukweli halisi wa hali ya kibinadamu.
Mwandishi wa Dw Anke Rasper alizungumza na Chirstina Bennet ambaye amefanya na Umoja wa Mataifa katika sekta ya kutoa misaada ya kibinadamu kwa zaidi ya muongo mmoja na katika mashirika kadhaa ya kimataifa.
Bennet amesema mkutano huo wa Istanbul ni muhimu licha ya kuwa kumefanyika mikutano mingi kuhusu kufikiwa kwa malengo ya meendeleo endelevu, kupunguza hatari ya kutokea majanga na kukabiliana na athari za mabadiliko ya hewa kwani kinachohitajika hivi sasa ni mtazamo wa kimataifa katika kutathmini changamoto zilizopo, hatua zilizopigwa na kinachohitajika kuboresha hali ya kibinadamu duniani.
Mfumo wa kutolewa misaada ya kibinadamu uliundwa miaka 75 iliyopita. Hata hivyo hii leo kuna majanga zaidi, mizozo na vita ina sura tofauti kwani mingi ni mizozo ya ndani ya nchi yanayohusisha makundi ya wapiganaji badala ya nchi dhidi ya nchi nyingine.
Mitazamo, mifumo, asasi za kushughulikia mizozo na suluhisho zilizokuwa mwaka 1945 imebadilika na haiwezi kutumika katika kuitatua mizozo ya nyakati hizi za sasa.
Wafadhili watakubaliana kutoa fedha zaidi na kwa upande wa mashirika ya kutoa misaada ya kibinadamu, yatakubali kuwa wazi na kuwjaibika zaidi kuhusu jinsi fedha hizo zinavyotumika.
Huku kukiwa na kiasi ya watu milioni 60 ambao wamelazimika kuyahama makaazi yao duniani na takriban wengine milioni 125 wanaohitaji msaada wa kibinadamu na ulinzi, washiriki wa mkutano huo wa Istanbul wanakubaliana kuna haja ya kuchukuliwa hatua za dharura kushughulikia majanga ya kibinadamu wakati huu kuliko wakati wowote ule.
Uturuki ambayo ni mwenyeji wa mkutano huo inawahifadhi wakimbizi milioni 2.7 kutoka Syria.
Mkuu wa kushughulikia masuala ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa Stephen O'Brien amesema hii ni fursa ya kipekee katika kizazi hiki kufikia ajenda zitakazoleta mabadiliko kuhusu namna ya kupunguza na kuzia mateso na mahangaiko ya watu wanaojikuta katika mizozo na katika hatari.
Umoja wa Mataifa umesema tofauti na mikutano mingine, huu haulengi kuchangisha fedha kuwasaidia waathiriwa wa mizozo na majanga bali ni wa kutafuta mkakati madhubuti wa kukabiliana na mizozo.
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel ambaye ni miongoni mwa viongozi wakuu wanaohudhuria mkutano huo wa Istanbul amesmea anatumai utapelekea kuwepo ushirikiano mzurti zaidi miongonbi mwa wahusika mbali mbali na kuwepo mtizamo mpya wa kushughulikia masuala ya kibinadamu.
Mwandishi: Rasper Anke/Caro Robi
Mhariri: Josephat Charo