Viongozi waomboleza kifo cha Kofi Annan
19 Agosti 2018Kiongozi huyo wa Umoja wa mataifa na mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel, na mwanadiplomasia nyota, Kofi Annan alifariki akiwa na umri wa miaka 80.
Raia huyo wa Ghana alikuwa kazi yake ni mwanadiplomasia ambaye aliongoza kwa heba ya kimya kimya na alipata sifa sehemu kubwa kwa kupandisha hadhi ya taasisi hiyo kubwa ya kimataifa katika siasa za dunia wakati wa vipindi viwili akiwa mkuu wa Umoja wa mataifa kuanzia mwaka 1997 hadi 2006.
Katibu mkuu wa kwanza kutokea katika eneo la Afrika kusini mwa jangwa la Sahara, Annan aliuongoza Umoja wa Mataifa katika miaka ya mtengano katika vita vya Iraq na baadaye alishutumiwa kwa rushwa katika kashfa ya mafuta kwa chakula , moja kati ya nyakati ngumu kabisa katika kipindi chake cha uongozi.
Familia imesema alifarikia kwa amani
Annan "kwa ustadi mkubwa aliuongoza Umoja wa mataifa katika karne ya 21 akielekeza ajenda muhimu ambazo ziliufanya Umoja wa mataifa kuwa na mwelekeo halisi wa amani, ufanisi na heshima ya utu duniani kote," mrithi wa Annan katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa , Ban Ki-moon , alisema katika taarifa.
Familia ya Annan ilisema kwamba alifariki kwa amani siku ya Jumamosi baada ya kuugua kwa muda mfupi.
Annan , ambaye aliishi si mbali na Umoja wa Mataifa katika makao yake makuu ya Ulaya mjini Geneva, aifariki hospitalini katika eneo linalozungumza Kijerumani la nchi hiyo, shirika la habari la Uswisi ATS limeripoti.
Katibu mkuu wa sasa Antonio Guterres amemueleza mtangulizi wake huyo kuwa, "ni nguvu inayoelekeza kwa ajili ya mambo mema". "Katika njia nyingi , Kofi Annan alikuwa Umoja wa mataifa," alisema.
"Alipanda kupitia ngazi mbali mbali na kuliongoza shirika hilo katika milenia mpya kwa heshima ambayo haina mfano na dhamira.
Desmond Tutu amesema Annan ni binadamu maarufu
Umoja wa Mataifa umesema utapepea bendera nusu mlingoti katika maeneo yake yote duniani kote siku ya Jumanne.
Na rais wa Ghana Nana Akufo - Addo alitangaza wiki ya maombolezo kwa kumkumbuka "mmoja kati ya raia mwenye hadhi ya juu kabisa".
Mwaka 2001, wakati dunia ikiwa katika mtafaruku wa shambulio la kigaidi la Septemba 11 nchini Marekani, Annan alipewa tuzo ya amani ya Nobel kwa pamoja na taasisi hiyo ya dunia "kwa kazi yake kuiweka dunia kuwa bora na iliyo na amani".
Mshindi mwingine wa tuzo ya amani ya Nobel , askofu mstaafu Desmond Tutu, amemueleza Annan kuwa "ni binadamu maarufu ambaye ameliwakilisha bara letu na dunia kwa neema, heshima na nidhamu.
Alizaliwa mjini Kumasi, mji mkuu wa jimbo la Ashanti nchini Ghana, Annan alifanyakazi kwa miongo minne katika Umoja wa mataifa na alikuwa mkuu wa kwanza wa taasisi hiyo akitokea katika shirika hilo.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe
Mhariri: Jacob Safari