1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi watatu wa Hamas wauwawa Gaza

Mjahida21 Agosti 2014

Wanamgambo wa Hamas wamesema kombora la Israel lililorushwa katika Ukanda wa Gaza hii leo asubuhi limewauwa makamanda wake wakuu wa kijeshi.

https://p.dw.com/p/1Cycw
Wanamgambo wa Hamas
Wanamgambo wa HamasPicha: Reuters

Shambulizi hilo lililotokea usiku wa kuamkia leo katika jengo moja la gorofa nne Kusini mwa mji wa Rafah, lilisababisha mauaji ya watu sita wakiwemo makamanda watatu wakuu wa kijeshi wa kundi la wanamgambo wa Hamas. Kundi hilo limethibitisha kuuwawa kwa Mohammed Abu Shamaleh, Raed Attar na Mohammed Barhoum.

Hii inaonekana kuwa pigo kubwa kwa kundi hilo huku ikiwa ni mafanikio muhimu kwa shirika la kijasusi la Israel.

Kwa upande wake jeshi la Israel limesema Abu Shamaleh alikuwa kamanda mkubwa kusini mwa Gaza aliyekuwa akitoa amri ya mashambulizi kwa wapiganaji katika vita vinavyoendelea. Attar anasemekana kushughulikia silaha za magendo kuingizwa Gaza na kusimamia uchimbaji wa mahandaki ya kuishambulia Israel.

Mwaka wa 2006 Attar alishutumiwa kuhusika katika kumkatamata mwanajeshi wa Israel Gilad Shalit kutokana na mashambulizi yaliofanywa kupitia mahandaki.

Shambulizi la katika Ukanda wa Gaza
Shambulizi la katika Ukanda wa GazaPicha: Mahmud Hams/AFP/Getty Images

Hata hivyo Israel haikuzungumzia chochote juu ya kamanda wa tatu aliyeuwawa Mohammed Barhoum.

Khaled Younis ni mkaazi wa Rafah anasema mashambulizi yanazidi na hali nayo inaendelea kuwa mbaya. "Saa nane na nusu asubuhi wakati tulipokuwa tumelala tulishambuliwa na roketi la kwanza kisha la pili la tatu na la nne, hatukuonywa kabisa tulishtukia tu nyumba imeshambuliwa sasa watu wanatafuta miili zaidi hali inazidi kuwa mbaya," Alisema Younis.

Rais Abbas ajitahidi kuendeleza mazungumzo yakusitisha mapigano

Shambulizi la Rafah limekuja siku moja baada ya jaribio la kumuua kiongozi wa kijeshi wa kundi la Hamas Mohammed Deif kufuatia shambulizi la angani katika nyumba moja aliyoshukiwa kuwepo kiongozi huyo. Mkewe na mtoto wake mchanga wa miezi saba ni miongoni mwa watu 19 waliouwawa katika shambulizi hilo la jana.

Licha ya mapigano yanayoendelea katika Ukanda wa Gaza rais wa mamlaka ya ndani ya Palestina Mahmoud Abbas anafanya mazungumzo nchini Qatar na kiongozi mkuu wa kisiasa wa Hamas aliye uhamishoni Khaled Mashaal, na mfalme wa Qatar Sheikh Tamim bin Hamad al-Thani. Kabla ya kuvunjika kwa mazungumzo ya kusimamisha mapigano Abbas alipanga kutumia wakati wa mazungumzo hayo kumuhimiza Mashaal na wenzake kuunga mkono pendekezo la Misri la kusitisha mapigano.

Rais wa Mamlaka ya ndani ya Palestina Mahmood Abbas na kiongozi wa Hamas Khaled Meshaal
Rais wa Mamlaka ya ndani ya Palestina Mahmood Abbas na kiongozi wa Hamas Khaled MeshaalPicha: Reuters/Thaer Ghanaim/Palestinian President Office

Hamas ilikuwa tayari imeshakataa kujihusisha na mpango huo, ikisema Israel bado haijajitolea kuyaheshimu makubaliano hasa katika hatua ya kusimamisha kuzingirwa kwa mpaka wa Gaza. Kuzingirwa kwa mpaka huo kulipendekezwa na Israel pamoja na Misri baada ya Hamas kuudhibiti Ukanda wa Gaza mwaka wa 2007.

Hadi sasa watu zaidi ya 2000 wameuwawa katika Ukanda wa Gaza tangu Israel iliponzisha oparesheni yake ya kuwasambaratisha wanamgambo wa Hamas mnamo Julai 8. Israel yenyewe imepoteza zaidi ya wanajeshi 60 katika mapigano hayo huku ikisema tayari imeshawaangamiza mamia ya wanamgambo wa Hamas.

Mwandishi: Amina Abubakar/AP/AFP

Mhariri: Josephat Charo