Vipimo vya DNA vyathibitisha kifo cha Prigozhin
27 Agosti 2023Katika kauli yake, msemaji wa kamati hiyo, Svetlana Petrenko ameeleza kuwa uchunguzi wa kijenetiki umeitambua miili yote 10 iliyopatikana katika eneo la ajali iliyotokea siku nne zilizopita.
Kamati hiyo haikutoa taarifa zaidi za ni nini hasa kilichosababisha ajali hiyo. Mapema wiki hii, mamlaka ya safari za anga ya Urusi, ilisema kuwa Prigozhin, pamoja na baadhi ya maafisa wake wa ngazi ya juu walikuwa katika orodha ya abiria na wahudumu waliokuwa kwenye ndege.
Soma zaidi: Putin avunja ukimya kuhusu kifo cha Prigozhin
Mmoja wa maafisa hao ni Dmitry Utkin, mtu anayetajwa kufanikisha operesheni za Wagner na anayedaiwa kuwa aliwahi kufanya kazi na shirika la Kiitelijensia la Urusi. Ndege iliyochukua uhai wa Prigozhin na maafisa wake ilikuwa ikisafiri kutoka Moscow kuelekea St. Petersburg kabla ya kupata ajali.
Tathmini ya kiitelijensia ya chunguzi wa awali wa Marekani iliionesha kuwa, mlipuko uliopangwa ndio uliosababisha ndege hiyo kuanguka. Kuliibuka pia mashaka kuwa Rais wa Urusi amehusika katika ajali hiyo jambo ambalo ikulu ya Kremlin ililikanusha kuwa ni uongo.
Kifo cha Prigozhin, aliyekuwa na miaka 62, kimetokea mieti miwili baada ya kufanya uasi dhidi ya jeshi la Urusi kitendo ambacho Rais Vladmir Putin alikiita kuwa ni "uhaini". Ikulu ya Kremlin ilifanya naye makubaliano ya kukomesha uasi huo.
Makubaliano hayo yalimruhuru kuendelea kuwa huru bila ya kufunguliwa mashtaka. Uasi huo wa muda mfupi ulionekana kuwa changamoto kubwa kwa utawala wa miaka 23 ya Rais Vladmir Putin.