1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Visa vya Covid-19 vyaongezeka pakubwa duniani

Hawa Bihoga
29 Desemba 2021

Maambukizi ya Covid-19 yamefikia rekodi katika muda wa siku saba, ambapo kwa wastani, visa zaidi ya laki tisa na 35 alfu vimegunduliwa kila siku kati ya Desemba 22 hadi 28, kulingana na takwimu za mamlaka za afya.

https://p.dw.com/p/44xdL
Deutschland | Coronavirus | Schnelltest
Picha: Peter Kneffel/dpa/picture alliance

Huku dunia ikirikodi jumla ya visa milioni sita na laki tano na hamsini kati ya Desemba 22 na 28, ambavyo vinawakilisha wastani wa visa laki tisa na 35 alfu na 863 kwa siku, kirusi hicho kinaelezwa kuenea kwa kasi ambayo haijawahi kushuhudiwa.

Takwimu hizo ni za juu kabisa kuliko rekodi zlizopita kati ya Aprili 23 hadi 29, wakati visa laki nane na kumi na saba alfu viliporekodiwa kwa wastani kila siku.

Visa vilivyogunduliwa ambavyo vimekuwa vikiongezeka tangu katikati mwa mwezi Oktoba, vimeongezeka kwa asilimia 37 katika muda wa siku saba zilizopita.

Shirika la Afya duniani WHO, limesema Jumatano kuwa kiwango cha ukuaji wa haraka huenda ni mchanganyiko wa uwezo wa kirusi aina ya Omicron kukwepa kinga na ongezeko la kasi ya uambukizaji wake.

Genf WHO Direktor Tedros Adhanom Ghebreyesus
Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Tedros Adhanom Ghebreyesus.Picha: DENIS BALIBOUSE/REUTERS

Shirika hilo la Umoja wa Mataifa limesema hatari jumla ya aina hiyo mpya ya kirusi inasalia kuwa juu.

Soma pia: Maambukizi ya Omicron Afrika Kusini huenda yamefikia kilele

Kwa sasa, mlipuko katika idadi ya visa haujasababisha ongezeko la vifo duniani, ambavyo vimekuwa vikishuka kwa wiki tatu zilizopita.

Karibu vifo vipya 6,450 kwa siku vimerikodowa kwa wastani katika muda wa siku saba zilizopita, idadi hii ikiwa ndiyo ya chini kabisa tangu Oktoba 2020.

Katika kilele cha janga hilo, vifo 14, 800 vilirekodiwa kila siku kati ya Januari 20 hadi 26 mwaka huu wa 2021.

Sehemu kubwa ya visa vipya vinatokea kwa sasa barani Ulaya, ambako zaidi ya visa milioni 3.5 vimerikodiwa katika muda wa siku saba zilizopita, sawa na wastani wa zaidi ya visa 510,000 kila siku.

Polisi Ujerumani waeleza kuchoshwa na maandamano

Nchini Ujerumani, taasisi ya magonjwa ya kuambikiza ya Robert Koch, RKI, imetangaza kugundua visa 10, 442 vya kirusi cha Omicron, na kwa mujibu wa taasisi hiyo kirusi hicho kina uwezekano mkubwa wa kuenea na kuwa kirusi kikubwa zaidi nchini humo. Jumla ya watu wanne wamefariki baada ya kugunduliwa na kirusi cha Omicron nchini Ujerumani.

Ujerumani imeanzisha masharti makali kukabiliana na kusambaa kwa virusi vya corona, lakini ukali wa masharti hayo ni wa wastani ikilinganishwa na hatua za awali.

Deutschland Würzburg l Polzeiaufgebot Nach Messerattacke
Polisi wa Ujerumani wakiweka ulinzi kuelekea moja ya maandamano ya kupinga hatua za kudhibiti maambukizi ya covid-19.Picha: Michael Probst/AP/picture alliance

Kampeni ya chanjo ya Ujerumani imeamshwa upya kwa chanjo za kuimarisha kinga, zinazofikiriwa kutoa ulinzi dhidi ya kirusi cha Omicron.

Hata hivyo, Ujerumani imeshindwa mpaka sasa kufikia lengo lake la kuwachanja asilimia 80 ya wakaazi wake, na kuahirisha lengo hilo hadi mwishoni mwa mwezi Januari. Karibu asilimia ya wakaazi, au watu milioni 58.9 wamepata dozi kamili za chanjo.

Soma pia: Wajerumani wazidi kupinga vizuizi vya COVID-19

Huku hayo yakijiri, chama cha wafanyakazi cha jeshi la polisi nchini humu kimeeleza hofu kwamba maafisa wa jeshi hilo wanakabiliwa na madhara ya kisaikolojia kutokana na kupelekwa mara kwa mara kwenye maandamano ya kupinga hatua za kudhibiti kuenea kwa virusi vya corona.

Mkuu wa chama hicho cha GdP Oliver Malchow amesema katika matamshi yaliochapishwa na shirika la habari la Redaktionsnetwerk Deutschland RND siku ya Jumatano, kwamba maandamano mengi yanayohusiana na virusi vya corona yanaweka uzito kwa vikosi vyao kutoka kwenye tukio moja na kupeleka jengine, na kwa sababu maandamano hayo pia yanahusisha makabiliano yanayozidi kuwa ya vurugu, yakiwa na viwango vikubwa vya uhasama dhidi ya maafisa wa polisi.

Chanzo: Mashirika