Visa vya homa ya nyani vyaongezeka mara tatu barani Ulaya
2 Julai 2022Kluge amesema katika taarifa yake kuwa jitihada za makusudi zinahitajika na kuyataka mataifa kuongeza juhudi na kuhakikisha kuwa ugonjwa huo hausambai kwa kasi. "Hatua za haraka na zilizoratibiwa ni muhimu ikiwa tunataka kukabiliana na kuenea kwa ugonjwa huu unaoendela", alisema Kluge.
Wiki iliyopita, WHO ilisema kamati yake ya dharura ilihitimisha kuwa kuenea kwa mlipuko wa ugonjwa huo kunatia wasiwasi, lakini bado haikutoa kibali cha kutangazwa kuwa dharura ya afya duniani
Hadi kufikia sasa visa 5,000 vya homa ya nyani vimeripotiwa katika nchi 51 duniani kote kulingana na kituo cha kuzuia na kudhibiti magonjwa cha Marekani. Asilimia 90 ya visa hivyo duniani vimeripotiwa katika nchi 31 za Ulaya. Watu wengi wameripoti dalili za kupata harara, homa, uchovu, maumivu ya misuli, kutapika na baridi.
Barani afrika nako hali ikoje?
Mamlaka za afya barani Afrika zimedai kuwa zinachukulia kuenea kwa ugonjwa huo wa Homa ya Nyani kama dharura na kuyataka mataifa tajiri kushirikiana upatikanaji wa chanjo katika juhudi za kuepuka kukosekana kwa usawa kulikoshuhudiwa wakati wa janga la mlipuko wa COVID-19.
Kaimu mkurugenzi wa kituo cha udhibiti wa magonjwa cha Afrika Ahmed Ogwell amesema kuwa "mlipuko huu haswa kwetu sisi ni dharura. Tunataka kuelezea Homa ya Nyani kama dharura sasa ili isiweze kusababisha maumivu zaidi na mateso".
Hadi kufikia sasa baadhi ya nchi za Afrika zimeripoti zaidi ya visa 1,800 vinavyosadikiwa kuwa vya Homa ya Nyani huku vifo zaidi ya 70 vikiripotiwa, lakini ni visa 109 pekee ambavyo vimethibitishwa maabara. Ugonjwa wa Homa ya Nyani umekuwa ukiwapata watu katika sehemu za kati na magharibi mwa Afrika kwa miongo kadhaa, lakini ukosefu wa uchunguzi wa maabara na ufuatiliaji hafifu unamaanisha kuwa visa vingi huenda havitambuliwi.
Kulingana na mkurugenzi wa WHO kanda ya Afrika, Dk. Moeti Matshidiso, ugonjwa huo umeenea katika nchi ambazo haukuwahi kuripotiwa hapo awali, zikiwemo Afrika Kusini, Ghana na Morocco. Lakini zaidi ya asilimia 90 ya maambukizi ya bara hilo yameainishwa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Nigeria.
Wanasayansi wanaonya kwamba mtu yeyote yuko katika hatari ya kuambukizwa homa ya nyani ikiwa atagusana kwa karibu, kimwili na mgonjwa aliyeambukizwa au nguo.
Wakati visa vya ugonjwa huo barani Ulaya na Amerika Kaskazini vikienea zaidi kwa wanaume wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja, hali ni tofauti afrika, ambako maambukizi yametoka kwa wanyama pori walioambukizwa kama vile panya au nyani.