1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Museveni aamuru watu wasitoke nje kukabiliana na corona

31 Machi 2020

Rais Yoweri Museveni wa Uganda ametoa amri ya kutotembea ovyo kote nchini kuanzia saa moja jioni hadi kumi na mbili asubuhi, ambayo ilitazamiwa kuanza kutekelezwa kuanzia usiku wa kuamkia leo (Jumanne 31 Machi).

https://p.dw.com/p/3aEKs
Yoweri Museveni
Picha: picture-alliance/dpa/A. Novoderezhkin

Hii ni mojawapo ya hatu ambazo zimechukuliwa katika kuepusha kuenea kwa virusi vya COVID-19 baada ya wagonjwa 33 kugunduliwa. Kipindi hicho kitachukua muda wa siku 14 kuanzia Jumanne.

Kwa jumla hata shughuli za kawaida mchana zimebanwa baada ya magari yote ya watu binafsi kupigwa marufuku kuendeshwa ila tu kwa dharura na idhini kutoka kwa mkuu wa wilaya.

Majengo ya maduka hayatafunguliwa isipokuwa tu shughuli za benki, ukusanyaji kodi na uuzaji wa vyakula katika masoko rasmi.

Akitangaza maagizo hayo siku ya Jumatatu jioni, Museveni aidha aliagiza viwanda kufunga kama haviwezi kuwaweka wafanyakazi katika kambi ya muda eneo la kazini kwao.

Katika hatua ya kuwapunguzia mzigo wafanyabiashara katika kipindi hiki, kiongozi huyo wa Uganda aliahidi kushauriana na benki, mashirika ya maji na umeme kutowaandama wanaodaiwa kwa sasa wala kuwakatia maji na umeme.

Aliahidi pia kutoa misaada ya chakula kwa familia zinazobainika kuwa husaka riziki zao za kila siku ili kujikimu chakula katika kipindi hiki ambapo Uganda inafanya juhudi kuepusha watu walioingia na virusi hivyo nchini kuwambukiza wengine.

Hata hivyo, Museveni aliwaonya wanasiasa kutojihusisha katika kutoa misaada yoyote kwa wananchi kwani wataweza kusababisha mikusanyiko, akitishia kuwa atakayepatikana akifanya hivyo atafunguliwa mashtaka ya jaribio la kufanya mauaji.

Lubega Emmanuel, DW Kampala