1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vita visivyokwisha vya makundi ya wanamgambo nchini Congo

Saleh Mwanamilongo
9 Septemba 2020

Asilimia sabini ya waasi wa kundi la FRPI,waliosalimisha silaha nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo wametoroka kwenye kambi waliokuwa wakipewa hifadhi.

https://p.dw.com/p/3iEe2
Wanamgambo wa kundi la FRPI kwenye kijiji cha Tchei,kusini mwa jimbo la Ituri.
Wanamgambo wa kundi la FRPI kwenye kijiji cha Tchei,kusini mwa jimbo la Ituri.Picha: Getty Images/AFP/L. Healing

Asilimia sabini ya waasi wa kundi la FRPI, waliosalimisha silaha nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo wametoroka kwenye kambi waliokuwa wakipewa hifadhi. Taarifa iliyotolewa leo na Radio Okapi ya Umoja wa Mataifa, inaelezea kwamba wapiganaji hao wamekimbia kambi ya Azita, kusini mwa mtaa wa Irumu, jimboni Ituri. Wanamgambo hao walisalimisha silaha mapema mwaka huu katika juhudi za amani, kufuatia mwito wa Rais Felix Tshisekedi. Shirika la kiraia la Walendu Bindi, linasema wapiganaji hao waliamua kurejea msituni baada ya kutopewa chakula na serikali kwa zaidi ya mwezi mmoja sasa. JeanClaude Katanga, kiongozi wa shirikala la kiraia la Baviba amesema serikali inashindwa kuwajibika katika kuwarejesha makwao wapiganaji hao. Mwezi Februari, serikali ya Congo ilitia saini mkataba wa amani na kundi hilo la FRPI, la wapiganaji wa kabila la Walendu ambao walitakiwa kujumuishwa katika jeshi la taifa. 

Ahadi zisizo tekelezwa

Baadhi ya wapiganaji  waliotegemea kutua chini silaha wamekata tamaa, huku idadi ya watu wanaokufa mashariki mwa Congo ikiongezeka.

Mwezi Juni, Umoja wa Mataifa,ulisema kwamba mnamo kipindi cha miezi minane iliyopita, watu zaidi ya 1,300 waliuliwa kwenye majimbo ya Ituri,Kivu ya kaskazini na Kivu ya kusini. Kwa mujibu wa wataalamu ni kwamba kuna  zaidi ya makundi 100 ya wapiganaji kwenye eneo hilo.

Mbunge wa Ituri, Gratien de saint-Nicolas Iracan amesema kuingia kwa wapiganaji walioshikilia silaha kwenye mji wa Bunia,Ijumaa iliyopita kunalenga kuiwekea shinikizo serikali katika kukamilisha mpango wa kuwaingiza jeshini wanamgambo hao.

Wanamgambo hao ambao wa kundi la wanamgambo wa kikabila la CODECO,limetuhumiwa kuhusika na mauwaji ya mamia ya raia.

Iracan amesema kwamba wanamgambo hao wameitaka serikali kuwapa fedha ikiwa imetaka watue chini silaha. Aliendelea kusema kwamba mpango wa amani wa rais Tshisekedi haujarahisisha watu hao kuweka chini silaha.

Rais Tshisekedi alifanya ziara yake ya kwanza jimboni Ituri mwezi Juni mwaka 2019.
Rais Tshisekedi alifanya ziara yake ya kwanza jimboni Ituri mwezi Juni mwaka 2019.Picha: Presidence RDC/Felix Tshiszkedi

Rais Tshisekedi aliwanyoshea mkono wapiganaji  tangu mwanzoni mwa muhula wake mwaka 2019. Lakini zaidi ya mwaka mmoja mwito huo haujazaa matunda na mauwaji yanaendelea kwenye majimbo hayo matatu.

Mwezi Ferbruari, wapiganaji wa kundi la Patriotic Front Resistance Force (FRPI) jimboni  Ituri, walitia saini mkataba na ujumbe wa serikali ya Kinshasa,lakini wamesema wanaendelea kusubiri utekelezwaji wa mkataba huo.

''Serikali haina mpango wowote madhubuti''

DR-Kongo MONUSCO-Friedenstruppen und Regierungsbeamte besuchen Dorf Kipupu
Picha: DW/Mitima Delachance

Kwenye jimbo jirani la Kivu ya Kaskazini,wapiganaji  485 wa kundi lingine linalojiita Nduma Defense of Congo-Renovated, NDC/R, walikusanywa kwenye kambi ya Rumangabo karibu na mji wa Goma baada ya kujisalimisha mwezi Agosti.Kiongozi wa kundi hilo, Desiré Ngabo amesema kwamba  walionyesha viongozi wa Kinshasa nia yao,lakini hadi sasa hakuna aliyewasiliana nao. Ngabo amesema kundi lake linapigana hasa na wapiganaji kutoka Rwanda wa kundi la FDLR.

Bertrand Bisimwa,kiongozi wa kundi la wapiganaji wa zamani wa M23 amesema kwamba serikali ya Congo haina mpango wowote madhubuti kwa ajili ya kufanikisha mwito wa rais Tshisekedi dhidi ya makundi ya wapiganaji.

Umoja wa Mataifa wapinga msamaha kwa wahalifu

Mtafiti wa maswala ya Congo, Christoph Vogel,amesema kwamba tangu mwaka 2019, kulikuwa na wapiganaji wengi wapatao elfu moja ,ambao walitua chini silaha  kwenye majimbo ya Kivu, lakini kutokuweko na uungwaji mkono wengi wao walirejea msituni.

Congo ina desturi ya kuwaingiza wapiganaji katika jeshi  tangu kutiwa saini kwa mkataba wa SunCity mwaka 2002 ambao ulikomesha vita vya pili nchini humo.

Vogel amesema Benki Kuu ya Dunia na nchi za magharibi zilichangia kwenye zoezi hilo miaka iliyopita.Lakini hadi sasa serikali ya Congo bado haijazitolea mwito nchi hizo kwa ajili ya mpango huu mpya.

Kongo, Kinshasa: UNO Mission in DR Kongo, Chefin Leila Monusco
Picha: DW/K. Tiassou

Makundi hayo ya wapiganaji huenda yakakata matumaini kufuatia pia kauli ya mkuu wa umoja wa mataifa nchini Congo. Leila Zerougui alifahamisha wiki iliyopita kwamba umoja wa mataifa unapinga kuweko na msamaha kwa wapiganaji na kuingizwa katika jeshi.

Umoja wa Mataifa uliunga mkono mkataba wa amani baina ya serikali ya Congo na kundi la wapiganaji la FRPI la jimboni Ituri. Mkataba huo unapendekeza kuweko na sheria ya msamaha kwa wapiganaji hao,lakini hawatohusishwa na msamaha huo wale waliofanya uhalifu wa kivita pamoja na visa vya ubakaji.