1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vita vya propaganda vyaielekeza Nigeria kubaya

Admin.WagnerD8 Oktoba 2010

Kauli ya Rais Goodluck Jonathan kwamba kundi la waasi wa Delta halihusiki na mripuko wa bomu uliotokea siku ya maadhimisho ya uhuru mwanzoni mwa mwezi huu wa Oktoba, imemuingiza kiongozi huyo vita vya propaganda

https://p.dw.com/p/PZmT
Rais Goodluck Jonathan wa Nigeria (aliyekaa kitako)
Rais Goodluck Jonathan wa Nigeria (aliyekaa kitako)Picha: AP

Ikiwa hata haujafika mwezi mmoja tangu Rais Goodluck Jonathan atangaze azma ya kutetea nafasi yake kwenye uchaguzi mkuu wa mwakani, tayari hali ya hewa imeanza kumuharibikia kiongozi huyo.

Maoni yake kwamba mripuko wa siku ya maadhimisho ya hamsini ya uhuru wa nchi yake, mjini Abuja, haukufanywa na kundi la waasi la Movement for the Emancipation of the Niger Delta, MEND, sasa yanamtumbukia nyongo.

Wapinzani wake wameyachukulia maoni haya kama ni kuwakingia kifua watu wa eneo lake la Kusini kwa gharama za watu wa Kaskazini. Jonathan ni Mkristo na mwenyeji wa Delta, na kabla hajawa makamo wa rais na baadaye rais, ndiye aliyekuwa gavana wa jimbo hilo lenye utajiri mkubwa wa mafuta.

Meli ya mafuta katika Niger Delta
Meli ya mafuta katika Niger DeltaPicha: AP

Serikali yake imekuwa ikionesha ishara za kumuhusisha mpinzani wake mkuu, Ibrahim Babangida, na mripuko huo. Babangida ni Muislam kutoka Kaskazini na aliwahi kuwa mtawala wa kijeshi wa nchi hiyo.

Tayari Jonathan anakabiliwa na upinzani kutoka ndani ya chama chake cha People's Democratic Party, PDP, ambapo baadhi ya wanachama wa ngazi ya juu wa chama hicho, wanamtaka kiongozi huyo aheshimu makubaliano yasiyo rasmi ya ndani ya chama, yanayotaka nafasi ya urais iwe ni ya kupokezana kati ya Kusini na Kaskazini ili kuondosha hisia za ukabila na udini.

Jonathan alirithi nafasi hii kutoka kwa Marehemu Umar Yar'adua, Muislam kutoka Kaskazini, ambaye alifariki mapema mwaka huu. Wanaomtaka Jonathan asigombee, wanasema kwamba, kwa vile Yar'adua alifariki kabla ya kipindi chake kumalizika, sasa bado inaendelea kuwa nafasi ya watu wa Kaskazini kutoa rais. Hoja hii inapingwa vikali na mwenyewe Jonathan, kwa maelezo kwamba haina uhalali wa kisheria wala wa kimaandishi.

Sasa, kutokea kwa mripuko huu na kuuhusisha kwake na kiongozi wa upinzani kutoka Kaskazini, licha ya wenyewe wapiganaji wa Delta kudai kuhusika nao, kumechukuliwa kwamba ni jitihada zake za kuua upinzani madhubuti dhidi yake ili hatimaye ajisafishie njia ya kushinda uchaguzi ujao. Jambo hili limewaudhi na kuwaunganisha watu wa Kaskazini dhidi yake.

Mwandishi wa habari wa gazeti la Next la nchini humo, Tolu Ogunlesi, amemfananisha Jonathan na mtu anayejipiga risasi kwenye mguu wake mwenyewe na kisha kujipakaza damu mdomoni mwake ili kuonesha kwamba ameonewa na kuwasingizia wengine uovu huo.

Tayari Babangida na wagombea wengine watatu wa wanafasi ya uraia kutoka Kaskazini, wametoa tamko la pamoja kumlaumu Jonathan kwa kulivua lawama kundi la MEND na kumshutumu kutumia mripuko huo wa bomu kama mbinu ya kuwatisha wapinzani wake.

Kundi jengine la wanasiasa kutoka Kaskazini linaloongozwa na waziri wa zamani wa fedha na mwanachama muanzilishi wa chama cha Jonathan cha PDP, Adamu Ciroma, limeyaita matamshi ya Jonathan kama fadhaa kwa taifa na likamtaka rais huyo ajiuzulu mara moja.

Hali hii ya kutokuaminiana iliongezeka hapo Jumaatatu iliyopita (4 Oktoba 2010), baada ya mkurugenzi wa kampeni wa Babangida, Raymond Dokpesi, kushikiliwa kwa muda mfupi na vyombo vya usalama vya Nigeria, ambavyo vilimuhoji kuhusiana na mripuko huo.

Wachunguzi wa mambo wanasema kwamba, ikiwa wanasiasa wa Nigeria hawakuepuka kutupiana maneno makali na kutishana hivi sasa, kuna hatari ya nchi hiyo, yenye wakaazi wengi zaidi barani Afrika, kutumbukia katika mgogoro mkubwa wa wenyewe kwa wenyewe.

Mwandishi: Mohammed Khelef

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman