Vita vya Yemen vyasababisha zaidi vifo vya watoto-UNICEF
12 Machi 2022Takriban watoto 46 waliuwawa au kujeruhiwa kwenye vita nchini Yemen katika kipindi cha miezi miwili ya mwaka wa mwaka 2022 wakati mapigano yakiongezeka kati ya vikosi vya serikali na waasi wa Kihouthi.
Hayo yameelezwa na afisa wa Umoja wa Mataifa Jumamosi,Phillippe Duamelle. Mwakilishi huyo wa shirika la kuhudumia watoto la UN nchini Yemen,amesema vita vimeendelea kuongezeka mwaka huu na kama ilivyo kila wakati watoto ndio wahanga wa mwanzo na wanaopata madhara zaidi.
Yemen inakabiliwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe tangu mwaka 2014 baada ya waasi wakihouthi kuudhibiti mji mkuu Sanaa na sehemu kubwa ya nchi hiyo upande wa Kaskazini,na serikali ikalazimika kukimbilia upande wa Kusini na kisha Saudi Arabia.
Muungano wa kijeshi unaopambana na waasi hao,ukiongozwa na Saudi Arabia uliingia YemenMachi 2015 ukiungwa mkono na Marekani na Umoja wa Falme za Kiarabu kujaribu kumrudisha madarakani rais Abed Rabbo Mansour Hadi.
Vita hivyo vimeongezeka tangu mwanzoni mwa 2022 wakati muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudia ulipojiimarisha na kuongeza hatua ya kuvisaidia vikosi vya kijeshi vya ardhini vya serikali ya Yemen kukabiliana na mashambulizi ya wahouthi katika mji wa Marib.
Mapigano yameongezeka pia katika sehemu nyingine za nchi hiyo ya kiarabu masikini kabisa duniani. Mwakilishi wa UNICEF Duamelle amesema vita hivyo vimesababisha watoto 10,200 kupoteza maisha au kujeruhiwa katika kipindi cha miaka miaka 7 na idadi kamili inawezekana kuwa kubwa zaidi.
Aidha ni vita vilivyosababisha pia mgogoro mbaya kabisa wa kibinadamu duniani.