1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vita ya Israel-Hamas:IDF yaripoti vifo vingi zaidi kwa siku

23 Januari 2024

Israel imeripoti idadi kubwa zaidi ya wanajeshi waliouliwa katika siku moja Gaza. Wakati huo huo, Waziri Mkuu Benjamini Netanyahu amesisitiza kuwa operesheni ya kijeshi ya nhi yake dhidi ya Hamas itaendelea hadi ushindi.

https://p.dw.com/p/4ba5T
Ukanda wa Gaza | Wanajeshi wa Israel | Picha imetolewa na IDF
Idadi kubwa ya vifo vya askari wa IDF inaweza kuongezea kasi ya miito kwa israel kusitisha mashambulizi.Picha: Israel Defense Forces via REUTERS

Israel imesema imeanzisha uchunguzi kuhusu kuuwawa wanajeshi wake jumla 24 huko Gaza. Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu amesema jeshi la nchi hiyo linachunguza kile alichokiita janga lililosababisha vifo vya wanajeshi wake hapo jana. 

Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu amesema jeshi la Israel limeshaanzisha uchunguzi lakini pia akasisizita kwamba wanapaswa kujifunza  na kuchukuwa hatua za kulinda maisha ya wanajeshi wake wanaopambana vitani.

Waliouwawa kwenye mashambulio ya jana Jumatatu huko Gaza ni jumla ya wanajeshi 24 wanaojumuisha 21 wa akiba.

Kwa mujibu wa msemaji wa jeshi, Daniel Hagari, kuuliwa wanajeshi hao ni pigo kubwa la wakati mmoja kuwahi kuonekana tangu vilipoanza vita vya ardhini Oktoba 27 na kwa hivyo jeshi la Israel linataka kubaini sababu ya mripuko uliowauwa wanajeshi wake.

''Bado tunafuatilia na kufanya uchunguzi wa yaliyotokea na kilichosababisha mripuko.''

Waziri Mkuu Netanyahu kwenye taarifa aliyoitowa leo Jumanne ameapa kwamba Israel haitositisha vita dhidi ya Gaza hadi itakapopata kile alichokiita ushindi kamili baada ya vifo hivyo vya wanajeshi wake wengi.

Herzi Halevi akiwa na makamanda walioko vitani Gaza
Mkuu wa majeshi wa Israel Herzi Halevi Picha: IDF/UPI Photo/Newscom/picture alliance

Mapigano makali yamepamba moto Kusini na katikati mwa Ukanda wa Gaza ambako wanajeshi wa Israel wamekuwa wakishambulia ngome za mwisho za watawala wa Kiiislamu katika Gaza.

Hivi sasa Israel inasema imeuzingira mji wa Khan Younis. Israel imekuwa ikijaribu kusafisha eneo zima hilo karibu na mpaka.

Vifo vya wanajeshi wa Israel vimeiumiza na kuikasirisha nchi hiyo, waziri wa Ulinzi Yoav Gallant amesema moyo wake uko pamoja na familia za wanajeshi hao waliouwawa katika kipindi hiki cha maumivu lakini pia akawahakikishia kwamba Israel haitorudi nyuma.

Na akaongeza kusema kwamba vita hivyo vya Gaza vitaamuwa mustakabali wa Israel wa miongo kadhaa ijayo na vifo vya wanajeshi wake vinapaswa kuwa chachu ya kufikiwa malengo ya nchi hiyo katika vita hivi.Mawaziri wa Umoja wa Ulaya waijadili hali ya GazaSoma pia: 

Msimamo wa Brussels

Hata hivyo Umoja wa Ulaya jana katika mkutano wake uliofanyika kwenye makao makuu ya baraza la umoja huo mjini Brussels uliitolea mwito Israel na Palestina kusitisha mapigano haraka huku taasisi hiyo ikiunga mkono suluhisho la kuundwa kwa madola mawili.

Mashambulio ya Israel Khan Yunis
Moshi ukifuka katika anga la mji wa Khan YunisPicha: SAID KHATIB/AFP/Getty Images

Waziri wa mambo ya nje wa Israel, Israel Katz na mwanadiplomasia wa ngazi ya juu wa mamlaka ya Wapalestina Riyad al Maliki walishiriki mkutano huo wa Brussels pamoja na mawaziri wa mambo ya nje wa nchi zote 27 wanachama wa Umoja huo.

Kadhalika mawaziri wa mambo ya nje wa Saudi Arabia, Misri, Jordan na katibu mkuu wa jumuiya ya nchi za Kiarabu nao walishiriki.

Mashambulio ya Wahouthi bahari ya Sham

Wakati huo huo, waasi wakihouthi wametowa onyo hii leo kwa Marekani na Uingereza wakisema mashambulio yao ya kijeshi yaliyofanywa dhidi ya ardhi ya Yemen usiku wa kuamkia leo hayatokaliwa kimya.

Nchi hizo zimefanya mashambulio katika mikoa ya Sanaa, Hodeida, Taez na Al-Bayda kwa muji wa msemaji wa kijeshi wa kundi la Wahouthi Yahya Saree.Soma pia: Israel yakabiliwa na shinikizo la kuafiki uwepo wa taifa huru la Palestina

Wahouthi wakifanya hujuma bahari ya Sham
Wahouthi Yemen walipoteka nyara meli ya Israel bahari ya ShamPicha: Ansarullah Media Centre/AFP

Waziri wa mambo ya nje wa Uingereza David Cameroon katika taarifa ya pamoja na Marekani amesema mashambulio hayo yamefanywa kujibu mashambulio yanayoendelea ya Wahouthi  dhidi ya meli za kimataifa za mizigo zinazopitia kwenye bahari ya Shamu:
''Tangu tulipochukuwa hatua siku 10 zilizopita kumekuwa na mashambulio zaidi ya mara 12 ya wahouthi  dhidi ya meli zinazopita bahari ya Shamu.Mashambulio haya sio halali na hayakubaliki na tulichokifanya tena ni kutuma ujumbe wa wazi kwamba tutaendelea kusambaratisha uwezo wao wa kufanya mashambulio haya na kuwapa ujumbe wa wazi kwamba tunatekeleza ujumbe wetu kwa vitendo.''

Wahouthi lakini wameapa kuendelea na mashambulio dhidi ya meli,hii ikiwa ni moja ya hatua zinazoonesha kuongezeka kwa mgogoro kwenye eneo hilo la Mashariki ya kati unaofungamana na vita vya Israel na Hamas na ambao unazidi kuibuwa wasiwasi katika kanda nzima.

 

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW