1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Raia waanza kupiga kura Bangladesh

Yusra Buwayhid
30 Desemba 2018

Raia wa Bangladesh wanapiga kura katika uchaguzi mkuu wa Jumapili ambapo Waziri Mkuu Sheikh Hasina atagombea muhula mwengine wa tatu katika mchuano dhidi ya chama kikuu cha upinzani ambacho kiongozi wake yuko jela.

https://p.dw.com/p/3Am9d
Bangladesch Wahlen
Picha: Reuters/M. Ponir Hossain

 Kuna matarajio makubwa kwa chama cha Hasina cha Awami League, kupata ushindi. Chama kikuu cha upinzani nchini humo cha Bangladesh Nationlist (BNP) ambacho kilisusia uchaguzi uliopita wa 2014, kimedhoofishwa safari hii baada ya kiongozi wake Khaleda Zia kuwekwa jela kwa makosa ya ufisadi.

Chama cha Zia mwenye umri wa miaka 74 na aliyekuwa waziri mkuu nchini humo kimesema mashtaka dhidi ya kiongozi wao ni njama za kisiasa.

Mtandao wa intaneti wa simu za mikononi umefungiwa na barabara za mji mkuu wa nchi hiyo zinaonekana kuwa tupu, kwavile wengi wamerudi katika miji walipozaliwa kwenda kupiga kura.

Wakati Zia akiwa jela, vyama vya upinzani vimeunda muungano unaoongozwa na Kamal Hossain, mwanasheria aliyesoma katika Chuo Kikuu cha Oxford Uingereza na mwanachama wa zamani wa chama cha Hasina cha Awami League.

Bangladesh Wahl  Sheikh Hasina
Waziri Mkuu wa Bangladesh Sheikh HasinaPicha: PID

Kampeni za uchaguzi huo ziligubikwa na madai ya upinzani ya kukamatwa na kufungwa kwa maelfu ya wafuasi wake. Watu zaidi ya kumi na mbili pia wameripotia kuuawa katika machafuko ya wakati wa kampeni za uchaguzi.

Wafanyakazi wa upinzani wanasema wanakabiliwa na mashambulizi na vitisho, ikiwa ni pamoja na kupigwa risasi na kukamatwa, hali iliyowazuia kuendesha shughuli zao za kampeni.

Idadi zaidi ya wapiga kur kuliko ya 2014

Pande zote mbili zinatarajia kuepusha kujirudia kilichotokea 2014. Zia na chama chake BNP walisusia uchaguzi na idadi ya watu waliojitokeza kupiga kura katika taifa hilo la Asia Kusini lenye watu milioni 160 ilikuwa ya asilimia 22.

Zaidi ya nusu ya viti 300 vya bunge la nchi hiyo vilikuwa havina washindani. Ushindi mkubwa wa chama tawala cha Awami League ulifuatiwa na machafuko yaliyosababisha watu 22 kuuawa. Mara hii watu milioni 106 wana haki ya kupiga kura, ikiwa ni pamoja na vijana wanaopiga kura kwa mara ya kwanza.

Chama cha Hasina kimekana madai ya upinzani na badala yake kujisifu kwa kujiamini na kusema kwamba rekodi yake nzuri ya kiuchumi itakipatia ushindi chama hicho.

"Sababu ya watu kukiunga mkono chama cha Awami League ni rahisi sana: maendeleo na ukuaji wa kiuchumi,"  mtoto wa kiume wa Hasina, Sajeeb Wazed, ameliambia shirika la habari la Reuters akiwa katika ofisi za waziri mkuu siku moja kabla ya uchaguzi.

Khaleda Zia Bangladesch
Kiongozi wa uinzani Bangladesh Khaleda ZiaPicha: Bdnews24.com

Ukuaji wa uchumi kwa mwaka umeongezeka kwa asilimia 7.8 katika mwaka 2017/18, ikilinganishwa na asilimia 5.1 ya mwaka 2008/09 wakati Hasina alipochukua madaraka ya nchi hiyo.

Hasina amesifiwa kimataifa kwa kuwapa hifadhi wakimbizi wa Kiislam wa Rohingya wanaokimbia ukandamizaji katika nchi jirani ya Myanmar, lakini serikali yake pia inakosolewa kwa kuukandamiza upinzani na kuwafunga wakosoaji wa serikali.

Kura zitaanza kuhesabiwa jioni na vituo vya televisheni vinatarajiwa kutangaza matokeo mapema Jumatatu.

Hasina na Khaleda wmekuwa wakipokezana uongozi kwa miongo mitatu iliyopita, na huu ni uchaguzi wa kwanza ambapo chama cha BNP kinashiriki uchaguzi bila ya Khaleda.

Mwandishi: Yusra Buwayhid/rtre

Mhariri: Iddi Ssessanga