Vituo vya wakimbizi vyafunguliwa rasmi Bavaria
1 Agosti 2018Leo Agosti Mosi katika jimbo la Bavaria hapa Ujerumani vimefunguliwa vituo 7 vya kuwapokea wakimbizi wanaofika Ujerumani.Vituo hivyo vinakusudiwa kuwahifadhi wakimbizi wanaosubiri maombi yao kuchunguzwa.Sauti za ukosoaji mkubwa zinatolewa dhidi ya waziri wa mambo ya ndani Horst Seehorfer juu ya kuanzisha vituo hivyo.
Wahamiaji wanaokuja kuomba hifadhi Ujerumani watawekwa katika sehemu moja kwenye kambi kubwa maalum zilizoanzishwa Bavaria. Kambi moja itawahifadhi wakimbizi hadi 1500 watakaoishi pamoja hadi pale watakapoifahamu hatma yao ya baadaye. Kwa maneno mengine mchakato mzima wa kuchunguza maombi ya kuomba hifadhi Ujerumani utafanyika wahamiaji hao wakiwa wanaishi katika kambi hiyo. Pindi mkimbizi atakubaliwa maombi yake atahamishwa na kupelekwa sehemu nyingine na ikitokea mkimbizi maombi yake yamekataliwa atalazimika kurudishwa moja kwa moja kutokea kambi hiyo ya pamoja.
Kwa mujibu wa waziri wa mambo ya ndani wa jimbo hilo la Bavaria aliyezungumza siku chache zilizopita na vyombo vya habari, Joachim Hermann katika maeneo yote vinakowekwa vituo hivyo saba vya wakimbizi, kutakuweko na matawi maalum ya idara ya uhamiaji ya shirikisho BAMF, idara ya masuala ya ajira sambamba na mahakama.
Vituo au kambi hizo saba maalum kwa ajili ya wakimbizi ambazo ni za majaribio zitadumu kwa kipindi cha takriban nusu mwaka na kisha itafanyika tathmini ya kwanza. Na mpaka wakati huo ndipo serikali kuu ya Ujerumani inaweza kuunda misingi ya kisheria kusimamia suala hili ambapo pia itategemea uungaji mkono wa serikali za majimbo ya Ujerumani. Mashirika ya kutetea wakimbizi yameikosoa hatua hii zikitolewa lawama kwamba uzoefu unaonesha kuwa wakimbizi wanaweza kuwekwa kwa muda mrefu sana katika kambi hizo bila kushughulikiwa.
Katika makambi ambayo tayari yako katika jimbo hilo la Bayern kuna zaidi ya watu 1000 wanaoishi kwenye kambi. Watu ambao hawana kitu cha kufanya na wala hawana mwelekeo wa kimaisha wanaishi pamoja katika hali ya msongamano na kutengwa kabisa na ulimwengu wa nje. Na hilo ndilo hasa linalokosolewa na mashirika hayo yanayosema kwamba asilimia 10 ya watu wanaoishi kambi ya Manching tayari wamewekwa katika eneo hilo kwa zaidi ya miezi 18. Ingawa kwa mujibu wa waziri wa mambo ya ndani wa shirikisho Horst Seehorfer katika hotuba yake aliyotowa mwezi Mei mbele ya bunge, hakuna mkimbizi atakayekaa kwenye vituo hivyo zaidi ya nusu mwaka.
Mwandishi:Felden Esther/Saumu Mwasimba
Mhariri: Josephat Charo