1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Amhara yawekewa vizuizi wakipinga mpango wa Ethiopia

11 Aprili 2023

Vizuizi chungumzima vimewekwa katika miji mitatu mikuu katika eneo la Amhara nchini Ethiopia, kufuatia maandamano ya kupinga hatua ya serikali ya kuvunja vikosi vya kikanda, ambavyo vimetuhumiwa kukiuka Haki za binadamu.

https://p.dw.com/p/4Pt2A
Äthiopien Bahir Dar | Friedlicher Protest gegen Premierminister Abiy
Picha: Alemenew Mekonnen/DW

Maandamano yameshuhudiwa katika miji kadhaa ya jimbo la Amhara tangu serikali ya shirikisho kutangaza siku ya Alkhamisi mipango ya kuvunja na kuunganisha vikosi vya kijeshi vya majimbo katika jeshi la shirikisho au idara ya polisi.

Katika mji wenye idadi kubwa zaidi ya wakaazi wa Gondar huko Amhara watu waliingia mtaani katika maandamano ya kupinga mpango huo wa serikali, huku wakaandamanaji wakipaza sauti "Abiy msaliti" na wakiapa kutokata tamaa kwa kile walichokiita kupingania haki ya Amhara."

Kulingana na taarifa zilizotolewa na mamalaka katika miji ya Gondar,Dessie pamoja na Debre Birhan ambako maandamano makubwa yameshuhudiwa huku waandishi wa habari wakizuiwa kuingia katika maeneo hayo kwa kile kilichotajwa ni sababu za kiusalama, vikwazo hivyo viliamriwa navikosi maalum vya usalama katika miji hiyo ikieleza kwamba usalama kwa sasa ni dhamana ya jeshi la shirikisho.

Soma pia:Umoja wa Mataifa wahofia ghasia zitaisambaratisha Ethiopia

Miongoni mwa vizuizi vilivyowekwa katika miji hiyo ni pamoja na kupiga marufuku usafiri wa umma wa pikipiki za magurumu matatu nyakati za usiku,huku sehemu za starehe ikiwemo baa na vilabu vya usiku vinapaswa kufungwa majira ya saa tatu usiku.

Marufuku nyingine imehusisha ubebaji wa silaha mbalimbali ikiwemo za jadi kama visu na vyuma, kufyatua risasi na fashifashi,kupigwa marufuku kwa migomo huku mikutano yoyote ya hadhara lazima itolewe taarifa kwa mamlaka.

Abiy:Sheria itatekelezwa dhidi ya upinzani haribifu

Waziri mkuu Abiy Ahmed mwishoni mwa juma alisema, mpango huo unania ya kuleta "Umoja wa Ethiopia" na kuonya kwamba hatua za kisheria zitatekelezwa dhidi ya upinzani wowote haribifu.

Äthiopien | Premierminister Abiy Ahmed Ali
Waziri mkuu wa Ethiopia Abiy AhmedPicha: Minasse Wondimu Hailu/AA/picture alliance

Vikosi hivyo vya kikanda vimezua utata hapo awali hasa wakati wa vita vilivyodumu kwa miaka miwili huko Tigray,huku vile vilivyoendesha oparesheni zake Amhara vilitoa msaada mkubwa kwa jeshi la shirikisho, lakini walilaumiwa kwa ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu.

Hata hivyo kwa mujibu wa katiba ya Ethiopia inaruhusu majimbi yake 11, yalioundwa kwa misingi ya kitamaduni na lugha kuwa na vikosi vyao vya polisi vya kikanda.

Soma pia:Marekani yagundua 'uhalifu wa kivita' Ethiopia

Lakini katika kipindi cha miaka 15 iliopita,baadhi wameanzisha vitengo maalum vya kijeshi ambavyo vinafanyakazi kinyume na katiba.

Hapo jana Chama tawala cha Prosperity, kilitoa tamko linaloelezea uvumi kwamba mpango wa kusambaratisha vikosi vya kikanda unahusu Amhara pekee kuwa ni uongo mtupu. Amhara ni kabila la pili kwa ukubwa na limetoa wasomi wengi wa kisiasa na kiuchumi.

Makubaliano ya amani kati ya serikali ya shirikisho na mamlaka ya Tigray yaliosainiwa Novemba 2022, yaliamsha chuki kali kwenye jamii ya wa Amhara ambayo kwa miongo kadhaa imehusishwa na mizozo ya kimaeneo huko Tigray.

Chama cha TPLF chawakabili wanajeshi wa Ethiopia Tigray